Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juma Kombo Hamad

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wingwi

Primary Question

MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:- Serikali imekuwa ikiendeleza zoezi la bomoa bomoa katika maeneo tofauti hapa nchini. Zoezi hili limekuwa likiwaathiri wananchi kiuchumi na hata kisaikolojia kwa kuwaacha wakiwa hawajui waelekee wapi:- Je, kwa nini Serikali isiwafidie wananchi hawa ukizingatia kwamba wakati wanajenga, Serikali ilikuwa inawaona, lakini haikuchukua hatua stahiki?

Supplementary Question 1

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Imekuwa ni jambo la kawaida kwa Serikali kuwaacha wananchi mpaka wamejenga na baadaye Serikali utakuta inachukuwa hatua sasa ya kubomoa nyumba za wananchi ambao tayari wamekaa pale kwa muda mrefu.
Je, haionekani kwamba sasa inaweza kupelekea matatizo kwa wananchi na kushindwa kujiweza na kujimudu kutafuta makazi mengine? (Makofi)
Swali la pili; je, ni lini sasa Serikali itasimamia Mipango Miji yake kama sheria inavyotaka kama ambavyo amekuwa akizungumza Mheshimiwa Waziri ili kuondoa tatizo hili?
Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza naomba kujibu kwamba, siyo kweli kwamba tunawaacha wananchi wanaendelea na kazi za kujenga bila kuwazuia. Tatizo lililoko ni katika Halmashauri zetu ambazo mara nyingi katika kutoa katazo mtu anapokuwa amekiuka wanaweka pengine alama ya X, lakini wakati huo huo pia wanaendelea na shughuli za maeneo mengine pasipo kufuatilia kwa karibu.
Mheshimiwa Spika, kwa hatua hiyo, Wizara kama Wizara, sasa hivi imechukua hatua na tumeanza na Mkoa wa Dar es Salaam. Tunapeleka usimamizi kwa viongozi wa maeneo hayo na ndiyo maana tumetoa pengine Ramani kwa Wenyeviti wa Mitaa ili aweze kutambua maeneo yake na mpango uliopo katika yale maeneo ili kuweza kujua lipi ni eneo la wazi, lipi ni eneo ambalo halitakiwi kujengwa?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna imani kwamba kama watatoa ushirikiano watakuwa ni sehemu ya usimamizi na hapatakuwa na mwananchi yeyote ambaye atakuwa amejenga kinyume cha sheria kwa sababu usimamizi tayari utakuwa chini ya viongozi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili nadhani limejibiwa pamoja na la kwanza kwamba ni lini tutafanya hivyo? Tayari hatua tumeshazianza. Natoa rai tu kwa sasa kupitia Bunge hili kwamba, tuombe Halmashauri zetu, kwa sababu maeneo mengi ambayo watu wanajenga kiholela; wapo wanaoona, wapo ambao wanakaa kimya na hawafuatilii.
Tuombe tu sasa kwamba popote pale ambapo mtu atajenga kinyume na utaratibu, halafu na uongozi wa pale upo unamwona mpaka anamaliza, atakapovunjiwa nyumba yake, kiongozi husika wa eneo lile atawajibishwa ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa yule ambaye amekiuka taratibu na yeye akiwa anashuhudia.