Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) aliuliza:- Kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuchukua maeneo kwa wananchi na kuahidi kuwalipa, lakini huchukua muda mrefu kuwalipa. Je, Serikali haioni kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima wananchi haki yao ya msingi?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Naibu Waziri pamoja na Waziri kwa jinsi ambavyo wanasimamia masuala mbalimbali ya Wizara hii vizuri, lakini pia nishukuru kwa haya majibu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya swali hili bado changamoto zipo, bado kuna watu wanaokiuka huu mwongozo wa Wizara. Sasa ningependa kujua, Wizara iko tayari kufanya utafiti ili kujua ni maeneo gani katika nchi hii, Mikoa gani, Wilaya zipi ambazo bado taasisi za Serikali, watu binafsi wanakiuka mwongozo huu wa Wizara na kuchukua hatua stahiki ili kuondoa hii kero kwa Wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ziko taasisi, ziko Halmashauri ambazo pia hazifuati utaratibu wa namna ya kuchukua maeneo ya wananchi. Kwa mfano katika jimbo langu, Kata ya Kirongo, Samanga, Kijiji cha Kiwanda, eneo la Mteri, Mkurugenzi alikwenda kuchukua ardhi ya wananchi ili kupata eneo la kujenga Ofisi ya Wilaya, lakini amewaacha wananchi katika malalmiko makubwa sana kwa sababu, hakuwahusisha kijiji, kata wala Halmashauri.

Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari ukipata nafasi uje Rombo ili twende pale tusaidie kutatua hili tatizo ili kuondoa hayo malalamiko kwa wananchi?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameongelea habari ya taasisi ambazo zinakiuka utaratibu, kwanza nipokee shukrani ya pongezi zake kwa niaba ya Waziri kwa Wizara, lakini pia nijibu swali lake ambalo ameongelea taasisi ambazo zinakiuka utaratibu kwa kukiuka.

Kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba pale ambapo inatokea taasisi yoyote au watu binafsi wanapotwaa maeneo kwa kukiuka utaratibu au mwongozo tulioweka tunaomba tupate taarifa mapema ili tuweze kuichukulia hatua kwa sababu si rahisi kuweza kujua kwamba wapi na wapi wamekiuka kama hatukuletewa taarifa. Kwa hiyo, mimi naomba hilo liweze kufikishwa ili tuweze kulifanyia kazi. Nitoe rai tu kwa taasisi zote kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa katika utwaaji wa maeneo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili amesema baadhi ya Halmashauri kutozingatia utaratibu wa kutwaa maeneo na akatolea mfano eneo la Kironga Somanga kule kwake.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa Halmashauri zote na tumeishatoa utaratibu, ni marufuku kutwaa ardhi ya mwananchi yoyote kwa sasa kama hakuna fidia ya kulipa. Kwa hiyo ni lazima kwanza fidia ipatikane ndipo uweze kutwaa ardhi, kwa sababu tumekuwa na changamoto nyingi kuna watu wengi wanadai fidia kutokana tu na taratibu zilikiukwa katika kuchukua maeneo. Kwa hiyo sasa hivi tumesema hatutaki kuongeza migogoro, unapotaka kutwaa ardhi ya eneo lolote lazima taratibu zizingatiwe na lazima kuwa na mazungumzo na wahusika wenye ardhi.