Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Kwa kuwa msimu wa pamba wa mwaka 2018/2019 ulikuwa na bei elekezi ndogo ya Sh.1,100 na kwa kuwa mara nyingi bei hizo elekezi zinapendekezwa kwa msukumo wa bei ya pamba duniani:- (a) Je, Serikali katika msimu wa mwaka 2019/2020 ina mkakati gani wa kuinua bei ya wakulima kutoka Sh.1,100 hadi Sh.2,500? (b) Kwa kuwa kuna Vyama vya Ushirika na Benki ya Wakulima, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la usambazaji wa mbegu za pamba katika Wilaya ya Bunda na hasa Jimbo la Bunda ambapo kila mwaka kunakuwa na uhaba wa mbegu na kutofika kwa wakati?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, nimshukuru kwanza Naibu Waziri wa Kilimo, Ndugu yangu Bashungwa kwa uadilifu wako, nadhani Mungu atakusaidia utafika unakoenda. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza la kwanza, na hili niliseme wazi kwa Waziri aliyopo na wewe mwenyewe, na kwa Wabunge wote nadhani unalijua hili, tatizo kubwa la pamba ni mambo mawili tu, la kwanza ni bei ya pamba, la pili ni usambazaji wa pembejeo kwa wakati ambao haufai.

Mheshimiwa Spika, suala la bei, naomba kujua kupata ufafanuzi, ni kwa nini sasa Serikali isitafute masoko ya ndani na masoko ya nje kwa wakati muafaka kwa msimu unaofaa, ili Wakulima wa pamba wapate bei nzuri ya kutosha?

Swali la pili kwa kuwa mwaka jana kwa msimu 2018/ 2019 Serikali ilikuja hapa Bungeni ikatuomba wakate shilingi mia kwa kilo ya pamba kwa wakulima, na lengo lilikuwa kupunguza au kufuta kabisa kero ya usambazaji wa mbegu za pamba au madawa kwa wakati muafaka, nini kimetokea mpaka leo Wakulima wa pamba wanateseka na mbegu hazipatikani kwa wakati na madawa hayapatikani kwa wakati, nini tatizo,? Tatizo ni ubovu wa bodi ya pamba? au ni mikakati mibovu ya Wizara ya Kilimo?

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Boniphace Getere kwa namna anavyohangaikia changamoto za Wakulima Jimboni kwake Bunda hususani zao la pamba.

Mheshimiwa Spika, tatizo la bei na usambazaji tayari Serikali chini ya mfumo wa ushirika tunaendelea kuimarisha ushirika ili ushirika uweze kuwajibika kwa Mkulima kwa kuhakikisha Mkulima anapata pembejeo kwa wakati anazingatia ubora na tayari Wizara yetu kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini ya Wizara tunaendelea kutoa elimu ili wakulima wetu wa pamba wazingatie kupanda kwa kutumia kamba ambayo ina vipimo.

Mheshimiwa Spika, pia, sambasamba na hilo usambazaji wa pembejeo hususani viuatilifu kwa misimu iliyopita vilikuwa vikichelewa lakini tayari Wizara tumeshakaa na kuhakikisha tuna mkakati wa kuhakikisha msimu huu viuatilifu vina wafikia wakulima wetu kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Getere ni kuhusu masoko ya ndani na nje nimuhakikishie Mheshimiwa Getere kwa vile ni mfuatiliaji mzuri tutakaa naye pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mikoa inayolima pamba na kuhakikisha tunakuwa tuna mfumo mzuri ambao utamuhakikishia mkulima kupata bei nzuri lakini na shilingi mia moja ambayo wanakatwa tutaangalia namna ya kuangalia mfumo mzuri ili makato ya mkulima yamsaidie katika kuwa na Kilimo cha tija, ili aweze kupata pato zuri katika msimu wa kuuza pamba, nashukuru.