Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Machano Othman Said

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Primary Question

MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. SALUM MWINYI REHANI) aliuliza:- Kambi za Jeshi za Ubago na Dunga zinawanyanyasa wananchi wa Shehia ya Kidimi kwa kuwataka waondoke katika maeneo hayo ambayo ni ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Ushirika kwa zaidi ya miaka 40 wameanza kupima na kuweka bikoni:- Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo na hatma ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo?

Supplementary Question 1

MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri majibu yake mazuri na ya ukweli, pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri aliahidi kulimaliza tatizo la Kambi ya Kisakasaka ambayo iko katika Wilaya ya Magharibi B. Je, ni hatua gani zimefikiwa hadi sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kambi ya Mtoni ambayo iko katika Wilaya ya Magharibi A ni ya muda mrefu na watu waliikuta kambi kabla ya kuhamia wao na kuna viashiria vya kuvamiwa na wananchi; Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini kuhusu suala hili na kama kuna upimaji au tayari imeshapimwa kambi ile ya Mtoni ili kuepuka uvamizi wa wananchi katika eneo lile?

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Kisakasaka ambalo tuliahidi kwamba tutamaliza tukiweza kupata bajeti, nieleze tu kwamba mpaka sasa fedha za ulipaji wa fidia na upimaji bado hazijapatikana, ni mategemeo yetu kwamba tunaweza tukapata kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha ili tuweze kulimaliza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kambi ya Mtoni ni dhahiri kwamba kambi karibu zote zimepimwa lakini kuna kuhuisha mipaka, kwa hivyo tutakachofanya kama nilivyoeleza awali ni kwamba tunatengeneza utaratibu maalum sasa wa kupitia maeneo yote ili tuweze kuhakikisha kwamba mipaka yetu inahuishwa na kuwataka wananchi wale ambao hawana stahili, basi waweze kutoka katika maeneo hayo, lakini wale ambao wataonekana na stahili aidha turekebishe mipaka au wapatiwe fidia zao ili tuondokane na migogoro ambayo imeonekana kwamba haiishi kati ya Wananchi na Wanajeshi. (Makofi)