Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHANCE M. GETERE aliuliza:- Mnamo tarehe 12 Januari, 2018 Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali katika Kijiji cha Mekomario – Bunda na katika msako huo wananchi wa eneo hilo waliharibiwa mali zao kama ilivyothibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda na kutangazwa kwenye vyombo vya habari yaani Star TV tarehe 15 Februari, 2018:- Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya kulipa fidia wananchi kutokana na uharibifu huo?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHANCE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wakati fulani hili Bunge haya majibu tunayopewa tuwe tunayachunguza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 12 ambayo wameisema hapa, ni kweli kulitokea vurugu na mimi kama kiongozi, Mbunge nilipiga simu saa 12.00 asubuhi kwa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuwataarifu kwamba kuna vijiji viwili vinagombania ardhi na kuna watu wameenda kulima, akina mama wawili wakanyang’anywa ng’ombe kwa upande wa pili, tulivyokuwa tumepewa taarifa hizo. Saa 12.00 asubuhi viongozi wote wa Mkoa na Wilaya wakasema wamepokea taarifa, Jeshi la Polisi limekwenda pale saa 11.00 jioni watu wamepigana mpaka wameuana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi msako uliofanyika saa 11.00 jioni, tarehe 13 tulienda pale viongozi wote, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa na vyombo vya habari vilikuwepo, maduka yote yamechukuliwa. Mambo mengine kusema hapa ni aibu, nachokiomba Serikali katika hili …
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu Serikali katika hili waende wakaangalie hiyo halisi ilivyokuwa na sisi tuna ushahidi wa kutosha juu ya jambo hilo. Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa chanzo cha mgogoro huo ni mgogoro wa ardhi ambao una vijiji vitatu ambapo kimsingi mgogoro ule ni kama umeisha. Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa aliyekuwepo Mheshimiwa Simbachawene alishafika pale akatoa maamuzi, maeneo yale yamegawanywa na vigingi vimewekwa. Ni lini sasa, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itaenda kuweka GN kwenye maeneo hayo ili kumaliza mgogoro huo?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba uniruhusu nimsifu sana Mheshimiwa Boniphance Mwita Getere. Eneo analoliongoza lina changamoto nyingi sana hususani hizi za kiulinzi na kiusalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, ombi lake aliloliomba, kwa sababu uchunguzi wa kipolisi bado unaendelea, haujakamilishwa kabisa, napenda nimhakikishie kwamba uchunguzi ule utaendelea kufanyika kwa kufuata taratibu za sheria za Polisi na sisi kupitia Kamati zetu za Ulinzi na Usalama, Mkoa na Wilaya tutafanya tathmini ya kina kuangalia matatizo gani yalijitokeza ili tuweze kuyatatua tukishirikiana naye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, uwekaji wa GN kuondoa migogoro iliyokuwepo kwenye vijiji husika, naomba sana Mheshimiwa Mbunge awe na subira, suala hili linafanyiwa kazi kwa ujumla kwa nchi nzima. Tulikuwa na migogoro zaidi ya 366 katika nchi nzima na tunaifanyia kazi kwa pamoja. Kwa hiyo, kuweka usuluhisho wa aina hiyo kwenye eneo moja tu la nchi, tunaomba sana Mheshimiwa Mbunge awe na subira tunalifanyia kazi kwa nchi nzima. Ahsante sana.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. BONIPHANCE M. GETERE aliuliza:- Mnamo tarehe 12 Januari, 2018 Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali katika Kijiji cha Mekomario – Bunda na katika msako huo wananchi wa eneo hilo waliharibiwa mali zao kama ilivyothibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda na kutangazwa kwenye vyombo vya habari yaani Star TV tarehe 15 Februari, 2018:- Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya kulipa fidia wananchi kutokana na uharibifu huo?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wabunge na Madiwani ni wawakilishi wa wananchi lakini mara nyingi baadhi ya Wabunge na Madiwani wamekuwa wakitoa taarifa za migogoro kati ya wananchi kwenye maeneo yao lakini matokeo yake ile migogoro inageuzwa Wabunge au Madiwani wanaonekana ni wachochezi wanakamatwa na kuwekwa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize Serikali, ni lini tabia hii itakoma Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wanapotoa taarifa ionekana kwamba taarifa hizo ni taarifa muhimu na za kufanyiwa kazi na ziheshimike? (Makofi)

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Vitongoji na Mitaa ni viongozi wa umma. Wanapotoa taarifa huwa zinapewa uzito unaostahili, isipokuwa tu kama kuna taarifa zingine ambazo zinakuja ku-counter kwamba labda wao wamehusika kwa njia moja au nyingine katika kusababisha mitafaruku iliyojitokeza hapo ndiyo hatua nyingine huwa inachukuliwa. Hata hivyo, taarifa zao huwa zinachukuliwa kwa uzito unaostahili na kwa heshima kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sema tu kwamba wenzetu wa Jeshi la Polisi kupitia Sheria ya Kanuni ya Adhabu wanao uwezo wa kufanya counter intelligence research kujua kwa kina tatizo hasa ni nini. Sasa wanaweza wakamshikilia kiongozi kwa muda ili waweze kupata taarifa za ziada, lakini kwa kweli kama watazidisha muda ambao wanaruhusiwa kukaa na viongozi kwa ajili ya mashauriano hiyo itakuwa wanafanya kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali lake ni la msingi na kwa kweli tutaliangalia kwa umakini zaidi ili kusudi kuweza kuweka mazingira mazuri zaidi. Sheria ya Kumlinda Mtoa Taarifa ipo na ilipitishwa na Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi wowote.