Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Primary Question

MHE. PHILIPO A. MULUGO aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kuipandisha hadhi Hospitali Teule ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki Dayosisi ya Mbeya iwe Hospitali Teule ya Wilaya ili wananchi wa Songwe waweze kupata huduma stahili?

Supplementary Question 1

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, amenitendea haki. Kwa kweli katika mwaka huu, leo nina furaha kubwa sana, kwanza Serikali imenipatia shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Songwe, nimefarijika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mwanzo wa mwezi huu alikuja Dkt. Kalindu kutoka Hospitali ya Mwambani kuleta tatizo hili kwa ajili ya kuteuliwa Hospitali Teule ya Wilaya. Kwa hiyo, Serikali leo imejibu kwamba imepandisha hadhi na mkataba wetu umekubaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja tu la nyongeza. Kwa vile sasa imekubaliwa kuwa hospitali ya wilaya, naomba kujua ni lini kibali kitatoka, maana ndiyo imekuwa hospitali ya wilaya lakini watumishi pale ni wachache na tangu mwaka 2014/2015 hatujawahi kupata vibali vya watumishi. Naomba nijue ni lini Serikali itatoa kibali cha kuajiri watumishi (madaktari na wauguzi) katika Hospitali ya Mwambani?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mwalimu Mulugo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu, naomba uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mulugo kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia suala hili. Alikuja Daktari kutoka Hospitali ya Mwambani lakini pia na juzi imekuja Kamati ya Siasa ya Wilaya yake nao wakawa wanaulizia suala hili. Kama ambavyo nilimuahidi tutafanya mapema na hili limewezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake anataka uhakika juu ya suala zima la kupata watumishi. Naomba nimhakikishie process ya ajira iko kwenye hatua za mwisho kabisa, zaidi ya wiki mbili tayari tutakuwa tushakamilisha suala la ajira na hakika tutahakikisha tunapeleka watumishi ili wakafanye kazi kwenye ile hospitali ambayo tumekubali itumike kama Hospitali ya Wilaya kwa sasa.