Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Wilaya ya Lushoto imezungukwa na misitu lakini misitu mingi imeungua kwa moto:- Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha uoto ule wa asili uliopotea kutokana na misitu kuungua?

Supplementary Question 1

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimsahihishe Naibu Waziri, amesema Msitu wa Mkussu; siyo Mkusu ni Mkuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa misitu ya Wilaya ya Lushoto iliyoungua tokea mwaka 2004 ni takribani miaka 14 sasa, lakini mpaka sasa hivi miti ile ya asili haijaota, imebaki vichaka tu. Je, nini commitiment ya Serikali juu ya kurudisha haraka uoto wa asili uliopotea kwa kupanda miti katika maeneo ya misitu iliyoungua pamoja na sehemu za maporoko? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Lushoto ina vijana wengi wamejiunga kwenye vikundi, je, Serikali ipo tayari kuwapa miche ya miti ya asili bure ili kurudisha haraka uoto wa asili uliopotea kwa muda mrefu sasa? (Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shabaani Shekilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukue nafasi hii kumpongeza sana kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sekta ya misitu na kwa jinsi ambavyo amekuwa akitoa ushauri kwa namna mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, eneo lolote lile ambalo ni misitu ya asili, ukienda kuanza kupanda miti mingine utaharibu ule uoto wa asili. Tunachofanya sisi ni kuliacha lile eneo kama lilivyo. Tukishaliacha kama lilivyo, ikifika kipindi ile miti itaota yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kabisa kwamba katika lile eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge anasema imechukua muda mrefu haijaota, lakini hivi sasa Wakala wa Taifa wa Misitu Tanzania wanafanya utafiti ili wapate mbegu na miche bora ile ya asili iliyokuwepo katika lile eneo ili tuone kama tunaweza tukaipanda katika eneo lile kusudi kurudisha ule uoto wa asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu miche hii ya asili ambayo inaweza ikapandwa katika eneo hili na wale vijana waweze kupata ajira, kama nilivyosema Wakala wa Taifa wa Misitu anafanya utafiti. Tukishakamilisha, tukabaini mbegu au miche mizuri ya asili katika eneo lile, basi tutaenda kuhakikisha kwamba inapandwa katika lile eneo na wale vijana watapata ajira.