Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:- Mheshimiwa Rais katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 aliahidi kujenga kilometa 10 za barabara ya lami katika Manispaa ya Moshi. (a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? (b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kusaidia Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kujenga mitaro katika barabara zake za lami ili kuzifanya zidumu muda mrefu?

Supplementary Question 1

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, kupitia fedha ya Mfuko wa Barabara na fedha ya Benki ya Dunia mtandao wa barabara ya lami katika Manispaa ya Moshi unaridhisha kwa kiwango fulani, lakini kwa kuwa fedha hizi hazina mahusiano ya moja kwa moja na ahadi ya Rais ya kilometa 10 aliyoitoa siku tano kabla ya kufunga kampeni zake mwaka 2015. Je, Waziri haoni kwamba, kuna sababu ya kumkumbusha Rais huenda akawa na nafasi ya kukumbuka ile ahadi yake ya kilometa 10 katika Manispaa ya Moshi?
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, tangu TARURA imeanza kazi Manispaa ya Moshi speed yake ya uwajibikaji haijaenda kwenye kasi ile ambayo Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ilikuwa inafanya wakati inasimamia barabara zake.
Je, Waziri haoni kwamba, kuna haja ya kuisukuma TARURA ili iweze kuongeza kasi ili kuhakikisha kwamba, barabara ambazo zimeharibiwa sana na mvua kipindi hiki cha mvua zinakarabatiwa, ili ziwe katika hali nzuri kama ilivyokuwa wakati Halmashauri ya Manispaa ya Moshi inasimamia yenyewe?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anasema kwamba utekelezaji wa hizi barabara hauna uhusiano wa moja kwa moja na ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, ni vizuri tu akatambua kwamba fedha zote ambazo zimefanya kazi ya ujenzi wa barabara katika Mji wa Moshi ni utekelezaji na mwenye fedha ni Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe. Najua ana kiu, angependa barabara nyingi zaidi zijengwe, lakini haiondoi ukweli kwamba tumefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa barabara katika Manispaa ya Moshi.
Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili, anasema haridhishwi na kasi ya chombo hiki ambacho tumeanzisha, TARURA, ukilinganisha na hapo awali jinsi ambavyo wao halmashauri walikuwa wakifanya.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie, chombo hiki ni baada ya kilio cha Waheshimiwa Wabunge wengi ambao tulikuwa tunapenda barabara zetu zichukuliwe na TANROADS, TARURA katika maeneo mengi inafanya kazi vizuri na Moshi naamini nao watafanya kazi vizuri. Hebu tukilee na tuhakikishe kwamba tunakisukuma tunakipa nguvu kifanye kazi iliyotarajiwa. (Makofi)

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:- Mheshimiwa Rais katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 aliahidi kujenga kilometa 10 za barabara ya lami katika Manispaa ya Moshi. (a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? (b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kusaidia Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kujenga mitaro katika barabara zake za lami ili kuzifanya zidumu muda mrefu?

Supplementary Question 2

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Halmashauri tano za Mkoa wa Dodoma zilipata fedha za kujenga barabara za mijini, lakini halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa hatukupata na nimezungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa kwamba Mpwapwa na Kongwa hatukupata barabara za kujenga mjini na ilikuwa ni ahadi ya Waziri wa TAMISEMI, tarehe 30 Desemba, Mheshimiwa Jafo.
Naomba maelezo ya Waziri kwa nini, Kongwa na Mpwapwa hatukupata hizi hela katika hiyo bajeti? (Makofi)

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yale yote na hasa kwa sababu na yeye amesema kwamba ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimhakikishie dhamira ya dhati ipo, lakini ni ukweli usiopingika kwamba miji mingine yote kwa Mkoa wa Dodoma imepata. Maana yake katika hatua inayofuata lazima tuhakikishe kwamba na maeneo hayo mawili ikiwepo eneo la kwako Mheshimiwa Spika yanatiliwa mkazo, ili barabara zijengwe kwa kiwango cha lami na kwa Mheshimiwa Lubeleje. Naomba nilichukue kwa mikono miwili kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba, na hasa kwa kuanzia kwa Mheshimiwa Spika hatukusahau hata kidogo. (Makofi)