Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:- Serikali inakusudia kuyaondolea hadhi ya uhifadhi baadhi ya maeneo ya hifadhi kwa kuwa yamepoteza sifa hiyo. Kwa mujibu wa kauli ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akihutubia huko Benaco Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera mnamo tarehe 22 Desemba, 2015. (a) Je, Serikali imeshaanza kuandaa mpango kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha kuwa kuna matumizi yenye tija na usawa baina ya wakulima na wafugaji pindi maeneo hayo yatakapokuwa huru ili kukuza uchumi na kuondoa hatari ya uvunjifu wa amani unaotokana na mgawanyo usio sawia kama ilivyo sasa? (b) Je, kama Serikali imeshaanza kuandaa mpango huo, ipo tayari kuzishirikisha mapema Halmashauri za Wilaya zitakazoguswa na jambo hili ili nazo zianze kufanya maandalizi ya suala hili kwa ngazi yao?

Supplementary Question 1

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ni miaka miwili na miezi minne sasa toka Serikali imetamka hilo ililolitamka kuhusu maeneo yaliyopoteza sifa mpaka leo na bado habari ya tathmini inazungumzwa mpaka leo, naomba Kauli ya Serikali kuhusu dhamira ya kukamilisha kazi hii ili tupeleke maendeleo kwa pamoja utalii, kilimo na mifugo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, asilimia 54 ya eneo la Wilaya ya Biharamulo ni maeneo yaliyohifadhiwa. Naomba kujua kutoka kwa Serikali, miongoni mwa maeneo yanayoonesha dalili za kupoteza sifa, yako yale yaliyozunguka Wilaya ya Biharamulo? Nakushukuru.

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Oscar kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kuwatetea wananchi wa Jimbo lake, hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kweli tathmini ilishakamilika katika hayo mapori tengefu 12 na tulishamaliza kazi. Kazi iliyobaki sasa ni kuhaulisha. Tararatibu za kisheria za kufuta yale maeneo lazima zizingatiwe. Kwa hiyo, huo ndio mchakato ambao bado unaendelea kwa hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu maeneo ambayo yanahusika katika Jimbo la Biharamulo; kwanza, kuna Masasi River, Biharamulo ambalo lina ukubwa wa kilometa 180 lipo kwenye orodha ya hayo mapori tengefu ambayo tunayaangalia. Lakini pia, kuna eneo lingine, Inchwakima nalo ni eneo ambalo bado tunaliangalia katika lile Jimbo la Biharamulo. Kwa hiyo, maeneo haya mawaili ndio yale ambayo yako katika mapori ya akiba ambayo tunayafanyia kazi, ili yaweze kurudishwa kwa wananchi pale ambapo utaratibu utakamilika.
Kwa hiyo, baada ya hapo naamini Mheshimiwa Mbunge utafurahi na wananchi wako watayatumia maeneo hayo vizuri na ipasavyo.