Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:- Hospitali ya Wilaya ya Mbulu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi; upungufu huo wa watumishi umeathiri utoaji wa huduma wa Hospitali hiyo na Vituo vya Afya vya Tawi na Daudi. • Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi katika Hospitali hiyo? • Serikali inatekeleza mpango wa upanuzi wa Vituo vya Afya zaidi ya 200 nchini; je, Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na changamoto za watumishi, fedha na vitendea kazi?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Mbulu, kwanza kuishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Daudi na Tlawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Kituo cha Afya cha Dongobeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba pamoja na shukrani hizi ninazotoa, naishukuru pia Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ambayo iko kwenye Halmashauri ya Mji wa Mbulu takribani shilingi bilioni moja na nusu katika bajeti ya mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili sasa; upungufu huu wa watumishi umepelekea watumishi waliopo kufanya kazi ya ziada kutokana na kwamba hospitali hii ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu iko mpakani mwa Halmashauri ya Babati, Halmashauri ya Karatu na Halmashauri ya Mbulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapokea huduma wa afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu, karibu asilimia 30 wanatoka kwenye maeneo ya pembezoni, hali inayopeleka watumishi walioko kufanya ya ziada.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali iniambie inachukua hatua gani sasa kuongeza fedha za OC kwa ajili ya wale watumishi wanaofanya kazi ya ziada ili waweze kuwahumia wananchi wetu wanaotoka ndani ya Halmashauri ya Mbulu na Halmashauri nyingine za jirani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa sasa fedha zinazotengwa za dawa na vifaa tiba ni kidogo kulingana na idadi ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini na kwa kuwa wale wanaotoka nje ya Jimbo la Mbulu Mjini hawapo kwenye mpango huu; Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa wa kutazama takwimu ya wananchi wanaopokea huduma ya Afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazipokea pongezi alizotoa kwa kazi ambayo inafanywa na Serikali, lakini ameuliza maswali mawili. La kwanza ni suala zima la kutoa allowance kwa wale watumishi wachache ambao wanalazimika kufanya masaa ya ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba kila Mtumishi na hasa wa sekta ya afya pale anapofanya kazi masaa ya ziada, ndiyo maana kuna kipengele cha on-call allowance ili waweze kulipwa stahili zao na wahakikishe kwamba wanafanya kazi ya kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba kibali cha kuweza kuwaajiri watumishi 25,000. Kibali hiki kitakapokuwa kimepatikana ni imani yangu kubwa Hospitali yao ya Mbulu nayo itapata watumishi kama ambavyo ameomba watumishi 91, ni ukweli usiopingika kwamba itapunguza uhaba uliojitokeza kufikia sasa hivi.

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:- Hospitali ya Wilaya ya Mbulu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi; upungufu huo wa watumishi umeathiri utoaji wa huduma wa Hospitali hiyo na Vituo vya Afya vya Tawi na Daudi. • Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi katika Hospitali hiyo? • Serikali inatekeleza mpango wa upanuzi wa Vituo vya Afya zaidi ya 200 nchini; je, Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na changamoto za watumishi, fedha na vitendea kazi?

Supplementary Question 2

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa matatizo ya Mbulu yanafanana kabisa na Halmashauri ya Mji wa Mafinga ambao kwa juhudi za wananchi pamoja na Serikali tunatarajia kukamilisha Kituo cha Afya cha Ulole, Kisada na Bumilahinga na pia Kituo cha Afya cha Ihongole kufuatia kupewa fedha shilingi milioni 500 na Serikali; lakini kwa kuzingatia kuwa Hospitali Mafinga iko kandokando ya barabara kuu na kati ya Iringa na Makambako hakuna hospitali hapo katikati.
Je, Serikali iko tayari kutuongezea idadi ya Watumishi ili tutakapofungua Zahanati na Vituo vya Afya hivyo, ufanisi wa kukaribisha huduma za afya kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga uwe wa dhati na wa vitendo?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, na wewe ni shududa kwamba wakati tunapitisha bajeti yetu Mheshimiwa Mbunge Cosato Chumi alikiri kabisa kwamba sasa hivi Mafinga ni motomoto kwa sababu kuna upanuzi wa hospitali. Pia hali iliyoko Mafinga ukilinganisha na Mbulu kuna utofauti mkubwa, maana wenzetu wana kituo. Kwanza kuna Chuo ambacho kinafundisha Waganga pale. Kwa hiyo, wakati wa kwenda kufanya practical inakuwa rahisi kwa wao kwenda katika Zahanati na Vituo vya jirani ikiwa ni pamoja Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba Vituo vya Afya vyote na Zahanati zote zinakuwa na wahudumu kwa maana ya Waganga pamoja na Wauguzi ili hicho ambacho kimekusudiwa na Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma kwa wananchi kinakuwa kweli na siyo nadharia.