Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Primary Question

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:- Je, kuvunjwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuna faida gani kwa wakazi wa Dodoma?

Supplementary Question 1

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Kakunda, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa Wakazi wa Dodoma wakiwemo Wabunge na Taasisi mbalimbali za Kiserikali kwamba ili waweze kupata huduma ya ardhi Manispaa ya Dodoma, basi kuna mzunguko mkubwa sana na mlolongo mkubwa sana.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kufanya uchunguzi maalum na kuchukua hatua kwa kuwa, sasa Manispaa ya Dodoma ni Mji Mkuu kwamba tunahitaji huduma hizi ziende kwa haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, zipo Taasisi za Serikali ambazo zinahamia Dodoma hivi sasa, zinataka kujenga ofisi zao hapa Dodoma, lakini bado kumekuwa na urasimu mkubwa sana taasisi hizo kupewa ardhi pale Manispaa.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuweka utaratibu maalum ili Taasisi hizi za Kiserikali ama Taasisi za Umma ziweze kupewa maeneo ya kuweza kujenga ofisi zao? (Makofi)

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma na ndiyo maana wakazi wa Kusini wanamwita mashine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlundikano wa kazi uliokuwepo katika kipindi hiki cha awali cha utekelezaji wa majukumu mapya ya kuunganisha majukumu ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma na ile iliyokuwa CDA ndio umefanya kuwe na baadhi ya malalmiko katika hatua za awali za utekelezaji wa kazi, kwa sababu kulikuwa na migogoro mingi sana ya viwanja, mahitaji ya kubadilisha mikataba mingi sana na hapo hapo kuna mahitaji ya kuendelea kupima maeneo mapya. Kwa hiyo, haya matatizo ambayo Mheshimiwa Maftaha ameyataja ni matatizo ya mpito tu ambayo yatarekebishwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, hadi sasa Manispaa imepima viwanja 1,288 na ambavyo tayari hati zake zimetayarishwa. Maeneo ambayo ni Mji Maalum wa Serikali yamepimwa viwanja 147, ikiwemo Ikulu, Wizara zote zimepatiwa hati na vilevile taasisi za umma na viwanja vya mabalozi 64.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nakuonesha hati ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni hii hapa, tayari imepatikana na ipo Ofisini. Wizara zote zina hati kama hii. Taasisi zote za umma ambazo zinahitaji ardhi, waende Manispaa pale watapewa hati zao ambazo zitawawezesha kupata maeneo ya kuweza kujenga ofisi zao haraka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika maeneo ya Nala wamepima viwanja 922 na kiwanja cha michezo cha Nzuguni kimepimwa, kile ambacho tulipata msaada kutoka Morocco na viwanja 218 katika maeneo mengine.
Waheshimwa Wabunge na wananchi kwa ujumla wanakaribishwa waombe viwanja Manispaa na mimi kama msimamizi wa Manispaa hiyo, nawaahidi kwamba watakuwa wamepata hati kabla ya mwisho wa mwezi huu wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limepimwa viwanja vya Serikali ni hili hapa na naweza nikalionyesha Waheshimiwa Wabunge waweze kuliona. Kazi imefanyika vizuri. (Makofi)

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:- Je, kuvunjwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuna faida gani kwa wakazi wa Dodoma?

Supplementary Question 2

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Dodoma sasa hivi ni Makao Makuu ya nchi na Manispaa wameongezewa jukumu lingine la ardhi ambalo lilikuwa la CDA, lakini kuna upungufu mkubwa wa vitendea kazi pale Manispaa hasa ile Idara ya Ardhi pamoja na watendaji ni wachache kiasi kwamba ukienda pale bado kuna watu wengi wanakaa kwenye foleni kwa muda mrefu.
Serikali sasa kwa kutambua kwamba Dodoma ni Makao Makuu, imejipangaje kuhakikisha kwamba Manispaa ya Dodoma inawezeshwa kwa vitendea kazi, miundombinu pamoja na watendaji wa kutosha ili wafanye kazi kwa weledi na kwa haraka? (Makofi)

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupata nguvu kazi ya kutosha kutoka kwenye ile iliyokuwa CDA, ni kweli kwamba bado kuna mahitaji ya watumishi na baadhi ya vitendea kazi na hivyo vinafanyiwa kazi mpaka mwezi wa sita, matatizo mengi yatakuwa yamekamilika.