Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:- Tatizo la kupotea kwa watoto katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa. Aidha, taarifa za kupotea kwa watoto hao zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari:- (a) Je, ni sababu zipi zinazochangia kuongezeka kwa tatizo hilo siku hadi siku? (b) Je, kwa nini taarifa za upatikanaji wa watoto hao hazitolewi kwenye vyombo vya habari? (c) Je, Serikali ina mkakati gani kuondoa tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kulitamka vizuri jina langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ambapo maswali ya msingi amenijibu vizuri na yameeleweka lakini kuna kifungu cha mwisho hapa ambacho kimenifanya niweze kupata maswali ya nyongeza. Amekiri kwamba watoto 184 walipotea na 176 wamepatikana na nane hawajapatikana lakini bado wanaendelea kutafutwa. Sasa napenda kumuuliza hivi Mheshimiwa Waziri kwa hao waliopatikana na hao waliokutwa nao, Serikali imechukua hatua gani ya kuwawajibisha kisheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wale watoto baada ya kupatikana ambapo alikuwa hayuko kwenye mazingira ya wazazi lazima afya itakuwa ni mgogoro. Je, Serikali au vyombo vimechukua hatua gani baada ya watoto hao kupatikana kupelekwa kwenye vyombo vya utibabu ili kuangaliwa hali yao na wazee kuweza kujiridhisha? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi kwamba, kupotea kwa watoto hawa 184 kulitokana na sababu mbalimbali ambapo miongoni mwa sababu hizo ilikuwa ni mazingira magumu ambayo wanaishi baadhi watoto, imani na kishirikina, visasi, kukosekana uangalifu wazazi/walezi na sababu nyingine ni kupotea kwa bahati mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sababu hizi ni tofauti na hatua ambazo zinachukuliwa zinategemea na sababu husika. Kwa zile sababu ambazo zimesababishwa na njia ya uhalifu basi hatua mbalimbali zimeshachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa watu ambao wamehusika na upotevu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbukuka juzi tu kulikuwa na tukio la kijana mmoja ambaye amejihusisha na utekaji wa watoto na kuomba fedha, kijana yule alikamatwa na kwa bahati mbaya alipata majeraha na akafariki. Nikuhakikishie kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi iko makini sana kuhakikisha kwamba inalinda watoto wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu hatua ambazo watoto hawa wanachukuliwa. Kama ambavyo nimesema kwamba kwa kuwa sababu ni tofauti kwa wale watoto ambao wamepatikana na madhara mbalimbali basi nao vilevile hufikishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya kuweza kupata huduma mbalimbali ili kuwaweka katika hali nzuri ya kimaisha na kiafya.