Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohamed Juma Khatib

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chonga

Primary Question

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB aliuliza:- Kumezuka wimbi kubwa sana lenye kutisha la ajali za bodaboda nchini kiasi cha kufanya hospitali zetu kupungukiwa na uwezo wa kuwahudumia waathirika wote wa ajali hizo. (a) Je, Serikali inaweza kulieleza Taifa sababu za kutokea kwa wingi kwa ajali hizo? (b) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na utitiri wa ajali hizo bila kuathiri ajira hiyo ya bodaboda?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Swali la kwanza naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, yeye mwenyewe amekiri hapo kwamba ajali hizi zinasababishwa na uzembe na wahusika kutofuata sheria. Lakini pamoja na kuelewa hivyo bado ajali zinaendelea kutokea na bahati mbaya sana ni kwamba ajali hizi zinawahusu nguvu kazi vijana wadogo sana wa Taifa letu.
Je, Serikali inafikiria njia gani nyingine ya kuwabana hawa kuhakikisha kwamba suala hili halitokei?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lingine, Mheshimiwa Waziri hamuoni kwamba inawezekana hawa vijana mbali na uzembe wanapata hizi leseni kwa njia ya rushwa? Kwamba wanafanya kazi hii bila ya ujuzi lakini ukiwafuata unakuta kwamba leseni wanazo. Je, Serikali itahakikisha vipi kwamba hawa vijana wote wanapata leseni kwa njia inayostahili?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa concern yake kwa sababu ni kweli jambo hili linagharimu maisha ya vijana wenzetu. Lakini niseme tu njia mbadala ambayo tumekuwa tukisisitiza ni kila familia na kila rika na kila vijiwe vya bodaboda kuchukulia kwamba jambo hili wana wajibu nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili si la Serikali peke yake kwa sababu Serikali imeweka taratibu zote hizi. Lakini ambacho huwa kinatokea kwa vijana wenzetu hawa anaweza akawepo mmoja anayemiliki leseni au anayemiliki pikipiki kwa taratibu zote, lakini anavyotoka na anavyokuwa kituoni, wanatokea wengine kirafiki wanapeana unakuta yeye hata mafunzo ya kuendesha bodaboda hiyo amejifunza ziku hiyo hiyo mpaka saa 4 asubuhi na inapofika mchana anabeba abiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu abiria anayepanda hamuulizi kwanza leseni yako iko wapi yeye anaona tu yuko na chombo mambo haya yanajitokeza. Na ndio maana tunapoona hayo yamejitokeza tunachukua hatua kali. Lakini msisitizo tunaofanya na tunapotoa mafunzo, tunaelekeza kila mmoja atambue kwamba hiki ni chombo cha moto na ukikiuka utaratibu wa matumizi yake una hatari ya kupata majeraha ama kupoteza maisha wewe mwenyewe pamoja na wale uliowabeba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu taratibu za leseni, kwa kiwango kikubwa tunafanya hivo. Sasa hivi kwenye kila Mikoa tumeelekeza taratibu za namna ya kuweza kupunguza hata athari za ajali zinapokuwa zimetokea kwa vijana wetu hawa kwa kuzingatia mahitaji yanayotakiwa katika matumizi ya vyombo hivyo vya moto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimewaelekeza hata wale viongozi wa vijiwe hivi vya bodaboda kuchukua wajibu wa kiuongozi kuelekezana kwamba hili jambo ni jambo linaloua, lakini vilevile wazingatie matumizi bora ya mahitaji ambayo yanatolewa katika uendeshaji wa vifaa hivo vya moto.

Name

Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB aliuliza:- Kumezuka wimbi kubwa sana lenye kutisha la ajali za bodaboda nchini kiasi cha kufanya hospitali zetu kupungukiwa na uwezo wa kuwahudumia waathirika wote wa ajali hizo. (a) Je, Serikali inaweza kulieleza Taifa sababu za kutokea kwa wingi kwa ajali hizo? (b) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na utitiri wa ajali hizo bila kuathiri ajira hiyo ya bodaboda?

Supplementary Question 2

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ajali hizi za wanaoendesha vyombo vya moto ni nyingi sana hapa nchini, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kila anayehitaji leseni anakuwa na bima ya afya ili waweze kurahisisha matibabu?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mchemba kwa concern hiyo ya vijana wetu, tumelipokea kama Serikali na tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Afya. Lakini kubwa si kwa anayehitaji leseni, tunaongelea kwa wale ambao wanafanya ile shughuli yenyewe. Kwa sababu kwenye leseni kuna kuwepo na vitu vya aina mbili, kuna yule anayemiliki na kuna wale wanaoendesha ambao ndio wamekuwa wakipata zaidi ajali kuliko wale wanaomiliki bodaboda zenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na viongozi wa vijiwe hivi tumeendelea kuwaelekeza kwamba wahakikishe katika makundi yale wanatambuana wale wanaohusika na akiongezeka ambaye hayuko kwenye kijiwe chao na hawajui kuhusu leseni zao, nao wachukue wajibu huo kwa sababu kwa kweli ni jambo ambalo linatoa ajira, lakini limekuwa likitugharimu sana maisha ya vijana wetu hawa wanapofanya kazi hizo.