Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:- Tathmini ya Mgodi wa Nyamongo (ACACIA) kwa wakazi wa Vijiji vya Nyakunguru, Kewanja, Nyangoto, Matongo kupisha upanuzi wa uzalishaji wa mgodi ilifanyika kuanzia mwaka 2012 ambapo wananchi walizuiwa kuendeleza maeneo yao:- (a) Je, Wananchi hao watapewa lini fidia kutokana na maeneo yao kulingana na bei ya sasa? (b) Je, fidia hiyo itaendana na usumbuu na hasara waliyoipata hadi sasa?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka niseme nimesikitika sana kwa majibu yaliyotolewa na Serikali na nataka niwahakikishie Bunge lako kwamba wananchi wa Tarime hawatakubaliana na hali hii. Nataka niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mhesimiwa Spika, katika sehemu ya kwanza ya majibu yaliyotolewa na Serikali, maeneo yote yaliyotajwa hapo, yalifanyiwa tathmini na mgodi wa North Mara na wakati fulani hivi baada ya tathmini, mgodi ulikwenda mbele zaidi kufyeka mazao ya wananchi na Mheshimiwa Spika kwa mujibu wa sheria ya madini, wananchi wanatakiwa wakae umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka eneo ambalo uchimbaji unafanyika.

Mheshimiwa Spika, wakati wote wananchi walipofanyiwa tathmini wamezuiliwa kuendeleza maeneo yao, mashamba yao yameharibika, nyumba zimebomoka na nyingi zimebomoka kutokana na blasting inayofanywa na mgodi lakini naambiwa hapa kwamba hawatalipwa wakati walifanyiwa tathmini.
Sasa swali langu ni hili, ni kwa nini mgodi ulifanyia tathmini nyumba, maeneo na mazao ya watu na kuzuia kuyaendeleza na sasa inasema kwamba haiwezi kulipa wakati ilifanyia tathmini yaani evaluation?

Swali la pili, haya majibu ya kukurupuka yasiyo na research, Serikali imesema kwamba wanalipa kwa mujibu wa viwango na North Mara inalipa fidia kubwa kweli kuliko ya Serikali, sasa mimi nina cheque hapa mbili za wananchi wa Tarime waliolipwa na haya ni matusi!

Mheshimiwa Spika, Nyamakaya Mbusiro amelipwa na Mgodi wa North Mara shilingi 3,871/= kama fidia ya shamba lake na nitawasilisha mezani kwako, cheque ya pili Chacha Muhabe Mwita amelipwa na Mgodi wa North Mara shilingi 7,273/= na ni nyingi mno, mashamba ya wananchi masikini. Nauli ya kutoka eneo la Nyamongo, Nyamwaga mpaka kufika Tarime Mjini ni shilingi 15,000/=.

Je, hii fidia ndiyo Serikali ya CCM inawaambia wananchi kwamba ni kubwa kuliko viwango ambavyo vinatakiwa kulipwa?

Name

Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Answer

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mambo ya fidia ya Nyamongo historia yake imeanza toka miaka ya 1980 na Mheshimiwa Mbunge atastaafu bado madeni yale yakiwepo. (Makofi)

Mimi mwenyewe nimekaa na wenyeji pale, kuna kitu kinaitwa ‘mtegesho’ na mtegesho umefanywa hata na wafanyakazi wa Serikali.

Kuna mtu anakuwa na nyumba, anamkaribisha mtu, watu wamejenga nyumba za thamani hata ya milioni 200 wakitegea mgodi uwalipe. Nimefanya vikao wakati ule na wenyeji wa Tarime, wenyewe baadaye wakasema hawa wenye mitegesho ndiyo wanakuja kuharibu taratibu za hayo malipo.

Kwa hiyo, hayo mashamba na hiyo ni kwamba tathmini ilifanyika na niliitisha kikao nikiwa na DC na wenyeji wananchi wa pale, nikaleta na wazee nikajaribu hata kuweka viongozi wa madhebu ya dini, Mheshimiwa Heche tumeongea naye nikasema baada ya Bunge suala la Nyamongo itabidi tuende tukae pale kama siku tano na itakuwa ya ukweli.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Heche asiondoke tutaenda, hayo mashamba saa zingine ni mtu anatafuta kaeneo, anaweka mimea usiku, asubuhi anataka tathmini ndiyo maana inakuja shilingi 3,000/=.

Kwa hiyo, kutatua tatizo la Nyamongo, itabidi mimi, Mheshimiwa Heche, DC, wale wananchi na viongozi wenyewe twende eneo moja baada ya lingine.