Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 2 Sitting 1 Energy and Minerals Wizara ya Madini 10 2016-01-26

Name

John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:-

Tathmini ya Mgodi wa Nyamongo (ACACIA) kwa wakazi wa Vijiji vya Nyakunguru, Kewanja, Nyangoto, Matongo kupisha upanuzi wa uzalishaji wa mgodi ilifanyika kuanzia mwaka 2012 ambapo wananchi walizuiwa kuendeleza maeneo yao:-

(a) Je, Wananchi hao watapewa lini fidia kutokana na maeneo yao kulingana na bei ya sasa?

(b) Je, fidia hiyo itaendana na usumbuu na hasara waliyoipata hadi sasa?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Wegesa Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi hawajaanza kulipwa fidia, ukweli ni kwamba fidia imeanza kutolewa na imelipwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kijiji cha Nyakunguru, awamu namba 24, awamu namba 34 na awamu namba 35 kijiji hiki kina ukubwa wa hekta 35. Makadirio ya fidia ilikuwa shilingi bilioni mbili, lakini ziliongezeka hadi kufikia bilioni ishirini na saba kutokana na ujenzi holela na upandaji wa mazao unaofanywa na baadhi ya wananchi wasio waaminifu wakati wa fidia ikifanyika maarufu inaitwa mtegesho.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, mgodi umeamua kuliacha eneo hilo na kutumia njia ya uchimbaji wa chini ya ardhi yaani underground mining method. Aidha, awamu namba 22 mheshimiwa spika, 23, 25, 28, 29, 33 na 44 yenye ukubwa wa eneo la hekta 90.4 ambao fidia yake ni shilingi bilioni 12 ililipwa kati ya mwaka 2012 na 2014.

Mheshimiwa Spika, kijiji cha Kewanja, awamu namba 30. Ukubwa wa kijiji hiki ni hekta 8.10. Makadirio ya fidia yalikuwa shilingi milioni 250 lakini kwa sababu ile ile ya ujenzi holela na upandaji wa mazao unaofanywa na baadhi ya wananchi wasio waaminifu, fidia pia iliongezeka kutoka shilingi milioni 200 hadi kufikia shilingi bilioni 8.3. Mgodi umeamua kuliacha eneo hilo kwa sababu hauna fedha ya kuwalipa, aidha awamu namba 26, 27 na 31 jumla ya hekta 26.8 zililpwa fidia ya shilingi bilioni 8.8.

Mheshimiwa Spika, kijiji cha Nyangoto, awamu namba 20, namba 36, namba 37, namba 38, namba 40, 41, 42 na 44, kijiji hiki kina ukubwa wa eneo wa hekta 115.79, jumla ya fidia iliyolipwa kwa mgodi huu ilikuwa ni shilingi bilioni 41.14.

Mheshimiwa Spika, ieleweke pia katika awamu ya 20, jumla ya hundi 157 zenye thamani ya shilingi bilioni 3.7 bado hazijachukuliwa na wafidia, baada yao kusingizia kwamba pesa hiyo waliyolipwa ni kidogo mno.

Mheshimiwa Spika, kijiji cha Matongo, awamu namba 39, mgodi ulihitaji eneo kwa ajili ya kinga ya kiusalama tu ambao ni Bufferzone ya mita hasa 200 wakati wa ulipuaji baruti kati ya eneo la mgodi na wananchi, lakini kwa sababu ya tegesha ile ile, mgodi uliamua sasa kuachana na eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, fidia husika hulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 zote za mwaka 1999. Fidia hii ni kulingana na thamani ya kipindi ambacho tathmini ilifanyika, lakini pia fidia hizi zilizingatia usumbufu na uharibifu wa mali za wadai husika. Aidha, wananchi wa maeneo hayo wanatakiwa kujua kwamba viwango vya fidia vinavyotolewa na mgodi wa North Mara ni vikubwa zaidi ya viwango vinavyowekwa na Serikali. Kutokana na ukweli huo, wananchi wote wanaotakiwa kuchukua fidia na kupisha shughuli za uchimbaji wanashauriwa sasa wachukue fidia ili kupisha shughuli za uchimbaji.