Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING aliuliza:- Hifadhi ya Kitulo ni muhimu sana kwa Taifa lakini mpaka sasa TANAPA haijaweka miundombinu ya hoteli na barabara ili kuwezesha watalii wanaokwenda Kitulo wawe na mahali pa kukaa:- (a) Je, ni lini Serikali itawezesha ujenzi wa hoteli ya kitalii katika Tarafa ya Matamba? (b) Je, ni lini Serikali itawezesha ujenzi wa barabara ya Chimala – Matamba – Kitulo ili kuinua utalii katika Hifadhi ya Kitulo?

Supplementary Question 1

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, naogopa majibu kama haya yasije yakarudiwa mwakani. Kwanza, nini kauli ya Serikali kufanya commitment ya ujenzi hasa wa barabara hii? Kwa sababu nafahamu Hifadhi za Ngorongoro, Manyara na Serengeti zina sifa kubwa kwa sababu ya miundombinu kuwa imeboreshwa na hasa ya barabara.
Pili, sambamba na hilo, Pori la Mpanga Kipengere, mipaka imerekebishwa kiasi kwamba inaumiza Kata za Ikuo, Kigala, Mfumbi, hivyo kusumbua wananchi kiasi kwamba hakuna hata eneo la kujenga miundombinu. Nini kauli ya Serikali kuhusu hili? Kwa sababu upande wa TAMISEMI najua wameshalishughulikia. Ahsante.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Profesa Norman King juu ya uwepo wa uwezekano wa kurudiwa kwa jibu nililolitoa leo. Nia njema ya Serikali kwanza ni kuhakikisha kwamba Hifadhi ya Kitulo inaboresha au Serikali inaboresha utalii kwenye Hifadhi ya Kitulo, siyo kwa faida ya Kitulo peke yake na wananchi wa Kata tulizozitaja na Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, lakini pia kwa ajili ya Taifa zima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Kitulo tunaiboresha kwanza kwa kuboresha miundombinu ya ndani ambako tayari tumeboresha barabara za ndani na mageti ya kuingia ndani ya hifadhi, nyumba za wafanyakazi pamoja na ofisi. Pia tumeboresha upatikanaji wa bidhaa za utalii. Kwa sasa hivi hifadhi hii ni maarufu kwa ajili ya maua na hali ya miinuko (terrain) ya pale na hali ya hewa ambayo inafanana tu na nchi nyingine za Ulaya tofauti na hapa kwa maana ya baridi ya muda mrefu na vitu vya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tayari tunataka kurudisha wanyama ambao walikuwepo zamani lakini baadaye kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujangili, wanyama hao wametoweka. Sasa tuna mpango wa kurudisha tena wanyama wakiwemo pundamilia, swala na nyumbu ili kuweza kuifanya hifadhi hii iweze kupanda hadhi, tuweze kupata watalii zaidi, ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza utalii kwenye eneo la kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba ni nia ya Serikali na kwa kweli tumepania kuweza kupandisha hadhi ya utalii, siyo kwa Kitulo peke yake, bali kwa utalii wa eneo la Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili; Mpanga Kipengere ni mojawapo ya maeneo ambayo tuna migogoro ya mipaka, lakini nataka kusema kwamba kama ilivyo kwa maeneo mengine kadhaa ambayo tumekwisha yaorodhesha, yanaendelea kushughulikiwa na Tume Maalum ya Serikali ambayo tumeiunda ya kushughulikia migogoro ya namna hii. Nafikiri tuwape muda mfupi tu ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii ilipata changamoto mbalimbali, mojawapo ikiwa ni ya kifedha, lakini sasa hivi tumetatua changamoto hiyo ya kifedha, wapo kazini na wanakwenda kwa kasi ili kuweza kutatua migogoro inayofanana na huu ambao uko pale Mpanga Kipengere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ziada tu namwomba Mheshimiwa Mbunge, baada ya session hii nikutane naye ili niweze kupata details za status ya Mpanga Kipengere ili niweze kuwashauri wale ambao wanaendelea na kazi hii kwa maana ya Kamati ya Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.