Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Augustino Manyanda Masele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:- Kwa kuwa Jimbo la Mbogwe limejaaliwa kuwa na madini ya dhahabu na utafiti umekuwa ukiendelea bila uchimbaji kufanyika katika maeneo ya Nyakafuru, Kenegere na kadhalika. Je, ni lini Wizara ya Nishati na Madini itayaachia maeneo haya na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo wadogo?

Supplementary Question 1

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kumuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa kampuni ya Resolute imekuwa ikifanya utafiti kwa muda mrefu ni lini sasa Serikali itaitaka kampuni hii iweze kufungua mgodi kwa ajili ya manufaa ya Wilaya hii ya Mbogwe?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, yapo mazungumzo baina ya Serikali pamoja na kampuni yanayoendelea kuhakikisha kwamba kampuni hii inaachia eneo la Kanegere ili kusudi wananchi waweze kupata maeneo ya kuchimba dhahabu. Ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atatembelea Mbogwe kuweza kuhakikisha kwamba jambo hili linaafikiwa? Ahsante.

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kampuni ya Resolute imekuwa ikifanya utafiti kwa muda mrefu na sasa hivi shughuli za utafiti kimsingi zimekamilika na hatua inayofata sasa ni kufungua mgodi. Kulingana sasa na taratibu za ufunguaji mgodi kampuni iko tayari kuanza kufungua mgodi miezi sita ijayo kutegemea sasa na bei ya soko la dhahabu pamoja na upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kutembelea eneo, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Masele anavyowatafutia maeneo wachimbaji wadogo. Hivi sasa katika eneo la jimbo la Mbogwe, Wizara imeshatenga maeneo yanayoitwa Shenda Kaskazini ambayo yana ukubwa wa hekta 990.99 na eneo hilo litapatiwa leseni 100 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa Mbogwe.
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hatua hiyo bado Wizara pia imezungumza na mwekezaji na kupata eneo lingine la Kanegere namba mbili ambalo litakuwa na ukubwa wa hekta 177 ambazo pia zitapatikana leseni 18.
Lakini kadhalika eneo la Bukandwe ambalo Mheshimiwa amelizungumzia pia kampuni imeachia eneo la ukubwa wa hekta 300 ambapo pia zinapatikana leseni kama 10.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Masele nimshukuru sana kwamba, wachimbaji wake watapata maeneo mengi na nitatembelea huko mara baada ya Bunge hili kuahirishwa.