Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatambua mchango mzuri wa wasimamizi wa Rasilimali Fedha, Wahasibu Viongozi (Chief Accountants) walioko kwenye Wizara na Idara za Serikali kwa kuwapandisha kwenye ngazi ya Ukurungenzi ili waweze kuleta tija zaidi kwa ushirika wao katika maamuzi ya Menejimenti ya Wizara/Idara zao?

Supplementary Question 1

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri sana nina swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, yapo maeneo machache viongozi hawa hawashirikishwi kikamilifu kutoa ushauri wa vifungu sahihi kwa matumizi kama ilivyoanishwa kwenye bajeti na kuathiri taarifa za fedha na kutekeleza hoja za ukaguzi. Je, Serikali iko tayari kutoa waraka, kusisitiza ushirikishwaji wa viongozi hawa wanaosimamia rasilimali fedha ili kuleta tija katika matumizi ya vifungu vya bajeti na kuboresha hesabu?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia matumizi mbalimbali ya rasilimali fedha, lakini niendelee kukumbusha tu kwamba mamlaka za ajira pamoja na menejimenti katika taasisi zote za umma, zinatakiwa kuhakikisha kwamba zinatumia fedha za Serikali kwa mujibu wa taratibu pamoja na sheria mbalimbali za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kusisitiza kwamba ni lazima waweze kushirikisha wakuu wote wa Vitengo, Wakuu wote wa Idara, katika menejimenti na vikao ili na wenyewe waweze kupata uelewa katika namna ambavyo mipango kazi ya taasisi inavyotekelezwa, pia waweze kutoa ushauri wao ni namna gani wanaweza kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao bila kuathiri taratibu mbalimbali za kifedha na sheria zinginezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Kwandikwa kwamba, kweli tuko tayari na baada ya kutoka tu hapa tutashauriana na Waziri wa Fedha ili kuona ni kwa namna gani sasa waraka unaweza ukaandaliwa, vilevile kwa upande wa utumishi kuweza kukumbushwa masuala haya.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatambua mchango mzuri wa wasimamizi wa Rasilimali Fedha, Wahasibu Viongozi (Chief Accountants) walioko kwenye Wizara na Idara za Serikali kwa kuwapandisha kwenye ngazi ya Ukurungenzi ili waweze kuleta tija zaidi kwa ushirika wao katika maamuzi ya Menejimenti ya Wizara/Idara zao?

Supplementary Question 2

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba eneo hili ni eneo muhimu sana katika utendaji wa Halmashauri zetu na ndiyo maana kumekuwa na Wakuu wa Idara wenye taaluma mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri anisaidie kitendo cha uteuzi wa Wakurugenzi kutoka nje ya wale Wakuu wa Idara na wakati mwingine watu ambao hawana taaluma kabisa ya kuendesha Halmashauri kuteuliwa kuwa Wakurugenzi katika maeneo haya na hata Waandishi wa Habari na maeneo mengine waliteuliwa ikaonekana kwamba ni form four na wakawa disqualified wakaondoka katika maeneo hayo na wengine wakaogopa kwenda kwenye maeneo waliyoteuliwa ……
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kitendo hicho cha kutoteuliwa wale Wakuu wa Idara kama sehemu ya promotion ni kuwavunja moyo katika utendaji wao wa kila siku?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafurahi kwamba yeye mwenyewe amesema ni promotion na hili ni suala la uteuzi. Teuzi hata siku moja haziombwi, mwenye mamlaka ndiye anayeamua amteue nani. Vilevile, kwa mujibu wa Ibara ya 36, Mheshimiwa Rais anayo mamlaka ya kumteua mtu yeyote ambaye anaona anafaa. Kwa hiyo, ni sahihi kabisa na naamini Mheshimiwa Rais ametenda haki kwa kufuata taratibu.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatambua mchango mzuri wa wasimamizi wa Rasilimali Fedha, Wahasibu Viongozi (Chief Accountants) walioko kwenye Wizara na Idara za Serikali kwa kuwapandisha kwenye ngazi ya Ukurungenzi ili waweze kuleta tija zaidi kwa ushirika wao katika maamuzi ya Menejimenti ya Wizara/Idara zao?

Supplementary Question 3

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa viongozi, wapo wanaokiuka taratibu za kuanzisha mashtaka katika utumishi wa umma, ikiwemo taratibu za uendeshaji wa mashauri ya nidhamu. Je, Waziri anatoa kauli gani kwa viongozi hao wasiotimiza wajibu wao?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati ambaye ametaka kusikia kauli ya Serikali tunasema nini kuhusiana na viongozi ambao wanakiuka taratibu katika uendeshaji wa masuala mbalimbali ya kinidhamu na uchukuaji wa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulie kusema kwamba kumekuwa kuna kauli nyingi kwamba watumishi wa umma wanakatishwa tamaa, watumishi wa umma wanakosa kujiamini na mambo mengine kutokana na hatua mbalimbali za kinidhamu zinazochukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba pamoja na malengo mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Tano, lengo mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunarejesha nidhamu katika utumishi wa umma, ikiwemo pia kuchukua hatua kwa watumishi wa umma ambao watakiuka sheria, kanuni na taratibu. Endapo mtumishi wa umma yuko katika mstari anatekeleza wajibu wake ipasavyo, sioni ni kwa nini kuwe na hisia au hofu. Niwahakikishie tu kwamba, Serikali yao iko pamoja nao na hakuna ambaye ataonewa bila kufuata taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema mambo yafuatayo:-
Taratibu nzima za kinidhamu zinasimamiwa na Sheria yenyewe ya Utumishi wa Umma, Kifungu cha 23(2), lakini kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kwa mujibu wa Kanuni ya 42, 47 na Kanuni nyinginezo, napenda kusema utaratibu mdogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hatua yoyote ya nidhamu haijachukuliwa ni lazima kuwe na hati ya mashtaka, ambapo mtuhumiwa au mtumishi huyo wa umma atapewa nafasi lakini vilevile katika hati hiyo atakuwa ameelezewa shutuma zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni lazima mtumishi wa umma huyo anayetuhumiwa apate haki au fursa ya kuweza kujibu hati hiyo ya mashtaka ambayo amepatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni lazima iundwe Kamati huru ya uchunguzi ambayo itampa fursa pia mtuhumiwa aweze kujibu au kukanusha tuhuma zilizoko chini yake. Vilevile kwa mujibu wa Kanuni ya 47 Mtumishi huyu wa Umma anayetuhumiwa atakuwa na haki ya kusikilizwa kikamilifu, atakuwa na haki ya kuweza kumhoji mwajiri, atakuwa na haki ya kuweza kuona vielelezo mbalimbali vilivyotumiwa katika kumshtaki. Pia Kamati hii sasa ya Uchunguzi, ziko ambazo zimekuwa zikikiuka taratibu, ni lazima ndani ya siku 30 baada ya kutoa uamuzi wake iweze kuwasilisha ripoti katika mamlaka ya nidhamu na ajira. Baada ya siku 30 tangu ambapo Kamati ya Uchunguzi imewasilisha ripoti yake ni lazima mamlaka ya ajira iweze kumjulisha mtuhumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mtuhumiwa atakuwa hajaarifiwa ndani ya siku husika, basi italazimika kuondolewa mashtaka na atakuwa huru kwa mujibu wa kifungu cha 48(9) cha Sheria ya Utumishi wa Umma. Nazitaka mamlaka mbalimbali za nidhamu kuhakikisha wanatimiza matakwa ya sheria hizi ili wasije wakawasababishia usumbufu watumishi wa umma vilevile wasije wakaisababishia Serikali hasara baadaye.