Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:- Je, Serikali imeweka mikakati gani ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini inayojengwa Mikindani Mtwara?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, NHIF wamekuwa wakitafuta viwanja kule Mtwara kwa ajili ya kujenga kituo kwa ajili ya kutolea huduma za kisasa. Kwa nini wasishirikishwe katika ujenzi huu wa Hospitali ya Kanda ya Kusini badala ya kufanya duplication ya kujenga huduma ambazo zinafanana?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa nini Serikali isitenge pesa zake yenyewe kwa kiasi cha kutosha ili kuhakikisha kwamba ujenzi huu unakamilika kwa haraka kwa sababu umeanza tangu mwaka 2009 na sasa hivi tuko 2016, ni karibia mika saba sasa. Je, wako tayari kutenga pesa zake za kutosha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 badala ya kuendelea na mazungumzo ambayo yanaonyesha kutokuzaa matunda?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii, pia namshukuru sana Dada yangu, Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini kwa maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana kwa jitihada anazofanya kufuatilia ukamilishaji wa mradi huu wa hospitali, yeye pamoja na Mheshimiwa Abdallah Chikota wamekuwa wakinisumbua sana kuhusu utekelezaji wa mradi huu.
Kwa msingi huo mimi mwenyewe nilifanya ziara kwenye mradi huu na mpaka sasa nimekwisha kufanya ziara mbili za kazi na katika ziara moja tuliongozana na wenzetu wa NHIF ambao ni Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa ambao upo chini ya Wizara yetu na kuwapa ushauri badala ya wao kujenga hiyo Center of Excellence ambayo wamekusudia kuijenga kule Kusini wafanye tathmini na watazame namna ya kutumia fedha zile ambazo walizikusudia kwa mradi wao kuwekeza kwenye kukamilisha mradi huu wa Hospitali ya Kanda ya Kusini, hivyo wazo lake na sisi tulikwishaanza kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lile swali la pili kwamba kwa nini Serikali haitengi pesa za kutosha kwenye bajeti yake; ni kwamba tayari mradi huu umekuwa ukitekelezwa kwa kasi kidogo na Serikali na majengo kwa sehemu kubwa ya kuanzia yamekwisha kukamilika yako takribani asilimia 95 kuanza kutumika na mimi katika ziara zangu nimewaelekeza namna ya kuanza utekelezaji wa mradi wenyewe hivyo hivyo ulipofikia kuliko kuusubiria mpaka ukamilike ili walau huduma za mapokezi, huduma za dharura lakini pia huduma za out patients (huduma za wagonjwa wa nje) zianze kutolewa kwa kutumia majengo ambayo tayari yanaelekea kukaimilika kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa tumekwisha kuwekeza takribani shilingi 1,782,000,000, na katika Bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali kwenye bajeti yake imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi kwamba tutaendelea kuitazama hospitali hii Ili kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 tuweze kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi huu.