Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Vibanda vya Wajasiriamali pembezoni mwa Barabara ya Njia Nane Kimara hadi Kiluvya utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Sita kwa kuwa msikivu sana kwa kilio cha wajasiriamali, Wilaya ya Ubungo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; kwa kuwa ni kawaida sana vinavyotengenezwa vibanda hivi vya wajasiriamali, wananchi mbalimbali kutokea kwenye maeneo mbalimbali ya nchi wanavamia na kusababisha walengwa kutofikiwa.

Je, Serikali au Wizara ya Ujenzi mko tayari kuiachia Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo kupanga wajasiriamali hao ili kufikia malengo tuliyotarajia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa mpaka sasa wajasiriamali wanateswa sana kupitia Wizara ya Ujenzi katika eneo lao la TANROADS katika maeneo haya waliyopo.

Je, Serikali ipo tayari kuchukua ombi la kuwaacha kipindi hiki wajasiriamali mpaka mradi utakapokamilika katika maeneo haya ya pembezoni mwa barabara? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Serikali nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nasema tu kwamba, kwa kuwa tunaowalenga ni wajasiriamali wa eneo husika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatafuta mpango mzuri ambao utahakikisha kwamba wale walengwa ndiyo wanaopata vibanda hivi. Ofisi ya Mheshimiwa Mbunge mhusika tutahakikisha kwamba inashiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kikubwa ambacho hapa tunaangalia ni kulinda usalama wa hawa wanaofanya biashara. Tunaweza tukawaacha wakaendelea kufanya biashara, lakini kukatokea madhara. Hata hivyo, nasema tu tumelipokea, tutatafuta namna nzuri ya kuona namna gani wanaweza wakafanya biashara bila madhara. Ahsante. (Makofi)

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Vibanda vya Wajasiriamali pembezoni mwa Barabara ya Njia Nane Kimara hadi Kiluvya utaanza?

Supplementary Question 2

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Jimbo la Kawe kama ilivyo Jimbo la Kibamba, lina wajasiriamali wengi sana barabarani. Kwa kuwa tuna barabara yetu kubwa kutoka Mwenge – Bagamoyo, kwa nini mpango huo mzuri wanaofanya Kibamba wasiulete pia Jimbo la Kawe ili wajasiriamali waweze kupangwa vizuri?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja tu ni kwamba, eneo hili la barabara hata wakati wa design yaani wakati inafanyiwa usanifu, hivi vibanda vinavyojengwa vilikuwa tayari viko kwenye usanifu. Sasa, itategemea na barabara kutoka Mwenge – Tegeta – Bagamoyo kama itakuwa ina design na eneo ambalo unaweza ukaweka vibanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tulichukue hilo kwamba katika barabara nyingi zinazodizainiwa mjini basi ni vyema suala hili la kuweka vibanda liwe limefanyiwa usanifu. Lisipofanyiwa usanifu halitawezekana kufanyika, ahsante.

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Katika kuongeza jibu alilojibu Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kwa namna ambavyo anapambana. Hapa kabla ya swali, amekuja kuniona kuhusu changamoto ya mafuriko ambayo ipo Barabara ya Mwenge kwenda Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemuahidi Serikali kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, tutakaa na kujipanga ili tuweze kwenda site na kuona cha kufanya ili kuwatoa wananchi kwenye adha ambayo Mheshimiwa Gwajima ameitaja. Ahsante sana.

Name

Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Vibanda vya Wajasiriamali pembezoni mwa Barabara ya Njia Nane Kimara hadi Kiluvya utaanza?

Supplementary Question 3

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, nakumbuka tulisaini Mkataba wa Barabara ya Mwendokasi inayoanzia Mwenge – Tegeta – Basihaya. Je, ni lini barabara hiyo ambayo Mkataba wake tumeshasaini itaanza kujengwa? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba tu kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri siku ya kusaini hiyo barabara mimi mwenyewe nilishiriki. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua iliyopo sasa hivi iko kwenye zile hatua za awali, yaani mobilization kwa ajili ya kuanza kuijenga hiyo barabara. Wakandarasi tayari wako wanafanya mobilization kwa ajili ya kujenga, yaani maandalizi ya awali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo, ahsante.

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Vibanda vya Wajasiriamali pembezoni mwa Barabara ya Njia Nane Kimara hadi Kiluvya utaanza?

Supplementary Question 4

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kama ambavyo ilivyo Kawe, Barabara ya Mafinga – Mgololo ambayo tulisaini Tarehe 26 mwezi Juni. Wananchi wananiuliza na juzi nilikuwa pale Kanisani pale Bwawani kwa Mzee Mahimbi, Wachungaji wakanivuta pembeni wakasema hii barabara inaanza lini? Ninayo majibu lakini wananchi wangetamani kusikia majibu ya Serikali.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mafinga – Mgololo ina urefu wa kilometa 81 na ni kati ya zile barabara ambazo zinatekelezwa kwa Mpango wa EPC+F. Hii barabara ndiyo ambayo ni ya kiuchumi ambayo karibu sehemu kubwa ya magogo na mbao zinapita kwenye hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumhakikishia kama nilivyosema kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Flatei, tayari wakandarasi wako site wanafanya usanifu wao wa kina na tunategemea kuanzia Januari watakuwa wameanza kazi hiyo. Kwa sasa wako wanaandaa maeneo ya kuchukua materials, maeneo ya kujenga hizo site zao na kama kutakuwa na uwezekano wa kuigawa hiyo barabara mara mbili ili waweze kuifanya hiyo kazi kwa uharaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, mradi huo upo na tayari wakandarasi wapo site japo hawajaanza ile earth work, yaani kazi ya kuanza kuchimba Barabara, lakini wako wanafanya maandalizi, ahsante.