Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 11 Sitting 29 Water and Irrigation Wizara ya Maji 383 2023-05-19

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, maeneo mangapi yameshabainishwa kuwa ni vyanzo vya maji salama ardhini na hatua gani zinachukuliwa kulinda maeneo hayo?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Bodi za Maji za Mabonde nchini na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ina jukumu la kutambua, kutunza, kuhifadhi na kuendeleza vyanzo vya maji vya juu ya ardhi na chini ya ardhi pamoja na kutambua uwezo wa chanzo na ubora wa maji yake. Hadi sasa vyanzo vya maji chini ya ardhi vilivyotambuliwa ni 152 na kati yake, vyanzo 30 vimewekewa mipaka na vyanzo 10 vimetangazwa kwenye gazeti la Serikali na hivyo kulindwa kisheria. Vilevile, Wizara inaendelea kufanya utafiti katika maeneo mengine 172 yenye maji chini ya ardhi ili kubaini uwezo wa chanzo na ubora wa maji yake.

Aidha, Serikali kupitia maabara za maji nchini hufanya ufuatiliaji wa mwenendo wa ubora wa maji chini ya ardhi kupitia visima vya uchunguzi vilivyochimbwa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Sampuli za maji huchukuliwa kutoka visima hivyo na kufanyiwa uchunguzi na pale inapothibitika kuwepo kwa mabadiliko ya mwenendo wa ubora hatua stahiki huchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kulinda maeneo yaliyotambuliwa kuwa vyanzo vya maji chini ya ardhi ikiwemo kuyawekea mipaka na kuyatangaza kwenye gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzani na uhifadhi wa maeneo husika.