Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 11 Sitting 22 Works, Transport and Communication Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 287 2023-05-10

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Primary Question

MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, kwa nini ilitumika njia ya single source kumpata Mkandarasi wa SGR Lot No. 6 Tabora – Kigoma na kusababisha hasara ya trilioni mbili?

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Manunuzi ya Umma imeainisha njia mbalimbali za manunuzi ya mkandarasi zinazoweza kutumiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na njia ya single source. Aidha, Manunuzi ya Mkandarasi kwa kipande cha Tabora - Kigoma yalifuata Sheria za Manunuzi ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 na Kanuni zake Na. 161 (1) (a) mpaka (c) (Single source Procurement for works) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013 na Marekebisho yake ya mwaka 2016.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa hakuna hasara yoyote iliyosababishwa na ununuzi wa mkandarasi wa ujenzi wa njia ya reli ya Tabora – Kigoma, bali ununuzi wa mkandarasi ulifuata taratibu zote za manunuzi ikiwemo majadiliano kwa lengo la kuhakikisha gharama sahihi za mradi zinapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, makadirio ya gharama za kihandisi (Engineering Estimates) yalikuwa dola za Marekani bilioni 3.066 sawa na shilingi trilioni 7.2 ikilinganishwa na gharama halisi za bei ya Mkandarasi (base price) baada ya majadiliano ambayo ni dola za Marekani bilioni 2.216 sawa na shilingi trilioni 5.2. Hii ni baada ya majadiliano yaliyookoa dola za Marekani milioni 273,913,703.25 sawa na shilingi bilioni 632.74 kutoka kwenye zabuni ya awali ya dola za Marekani 2,490,124,575.00 sawa na shilingi trilioni 5.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa utaratibu wa manunuzi kwa njia ya Single source ndiyo uliotumika kumpata Mkandarasi YAPI MERKEZI wa Ujenzi wa kipande cha tatu kutoka Makutupora kwenda Tabora, na Kipande cha nne, yaani Tabora - Isaka, ambapo gharama zake ni dola za Marekani bilioni 2.213 sawa na Shilingi za Kitanzania trilioni 5.19, ahsante.