Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 34 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 296 2018-05-22

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO (K.n.y. MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO) aliuliza:-
Kuna upungufu wa magari katika Vituo vya Polisi Mkoa wa Ruvuma. Yaliyopo sasa ni mabovu kabisa na hayafanyiwi matengenezo kutokana na ukosefu wa fedha.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari kwenye vituo hivyo?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka pesa kwenye vituo hivyo kwa ajili ya matengenezo ya magari na mafuta ya magari hayo ili polisi waweze kufanya kazi zao kwa wakati?

Name

Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama lilivyoulizwa kwa niaba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Ruvuma una jumla ya magari 33 na kati ya hayo magari 24 ni mazima yanafanya kazi na magari tisa ndiyo mabovu. Aidha, Jeshi la Polisi hufanya mgao wa magari katika mikoa na vikosi kwa kuzingatia vigezo mbalimbali kama kiwango cha uhalifu katika eneo husika, hali ya jiografia, idadi ya watu na mahitaji ya kiutawala ambapo katika mwaka 2015 Mkoa wa Ruvuma ulipokea magari 11. Hivyo, mpango wa kupeleka magari katika Mkoa wa Ruvuma utategemea upatikanaji wa magari mapya na mahitaji kulingana na vigezo vilivyoainishwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga na kupeleka mgao wa fedha katika Jeshi la Polisi kila mwezi ambapo fedha hizi hugaiwa na kupelekwa mikoani kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya jeshi ikiwemo operation, matengenezo ya magari na mafuta kwenye vituo vya polisi. Aidha, utaratibu ulipo sasa kila Mkoa unapelekewa fedha kwa ajili ya matengenezo na mafuta kila mwezi kupitia kasima ya mikoa. Ni kweli kuwa magari mengi kwa sasa yamekuwa ni ya muda mrefu hivyo huhitaji matengenezo ya mara kwa mara ambapo Jeshi la Polisi linahitaji kufanya matengezo kwa magari yanayoharibika kwa kutumia fedha zinazopelekwa na kuwashirika wadau wa ulinzi na usalama katika maeneo husika.