Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nicodemas Henry Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo katika Wilaya ya Mbogwe?

Supplementary Question 1

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu hayo, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo kwa wawekezaji, wanakuja na leseni sehemu ambapo wanachimba wachimbaji wadogo, wakifika na leseni wanawafukuza bila kuwalipa fidia wamiliki wenye maeneo (ardhi): Sasa nataka kujua, nini kauli ya Serikali kuhusu hawa waliomiliki ardhi yao kwa muda mrefu wanafukuzwa pasipo kupewa malipo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Wachimbajii wadogo wamekuwa na kilio kikubwa cha tozo kwenye mifuko ya mawe: Ni lini Serikali itawapunguzia tozo ya mawe kwenye maduara pale wanapochimba ili kusudi nao waweze kufaidika na kazi zao? (Makofi)

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Answer

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maganga, Mbunge machachari wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ieleweke kwamba uchimbaji wa madini, ili mtu aweze kuchimba ni lazima awe na leseni ya uchimbaji madini. Kabla hatujatoa leseni kwenye eneo lolote, timu yetu ya wataalam lazima ikague maeneo hayo kujiridhisha nani yupo? Anafanya kazi gani? Kama hawajaomba maeneo hayo, mara nyingi huwa tunawakumbusha kuomba. Inapotokea anatokea mtu amepewa leseni kwa kawaida, na hata Mbogwe tumefanya hivyo; wale waliopewa leseni lazima waingie makubaliano na wenyeji ili kusionekane kuna upunjaji wa namna yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu tozo za mifuko, jambo hili ni jambo ambalo linawezekana kufanyiwa kazi kama tu aina ya uchimbaji unaofanyika utakuwa wa nia ya kuchimba, kuchakata na kuzalisha dhahabu. Ila, kama wachimbaji wenyewe wataamua kugawana mawe, na ni uchimbaji usiokuwa rasmi kwenye rashi, wajue kwamba na Serikali lazima iwe na sehemu ya mgao kwenye migao hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Name

Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo katika Wilaya ya Mbogwe?

Supplementary Question 2

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Wanawake wengi sasa hivi wameanza kujiingiza katika biashara ya madini: Nini mkakati wa Serikali katika kuendeleza wanawake hawa kwa kuwapatia mikopo na kuwahamasisha wanawake wengi zaidi waweze kushiriki katika biashara ya madini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Answer

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubali kwamba katika watu ambao wamechangamkia fursa ya uchimbaji madini, kundi kubwa la wakina mama wameingia kwenye uchimbaji madini. Mahali ambako wanawake wanachimba, tuna uzoefu, ni watu waaminifu, wanaolipa kodi kwa wakati, hawahitaji kusimamiwa na Polisi; na hata mirabaha ambayo tumewapa kusimamia, wao wameonesha bila shaka yoyote kwamba ni watu wanaoweza kujisimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi Serikali tunaangalia utaratibu bora zaidi wa kuwapatia wachimbaji mikopo wakiwemo na wanawake. Tunachohitaji ni muda wa kufanya study. Kwa sababu kinachowekwa kama dhamana ya kuchukulia mkopo, tungetamani iwe hiyo leseni yenyewe ambayo mchimbaji anapewa. Kwa hiyo, tunalikamilisha ili tufanye kwa namna ambayo hatutakosea kama tulivyowahi kukosea huko nyuma, kuwapatia watu mikopo na baadaye watu hao wakapotea na fedha zenyewe.

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo katika Wilaya ya Mbogwe?

Supplementary Question 3

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri anajua Bunda kuna wachimbaji Kamkenga na Kinyambwiga naye amefika. Sasa sisi kule wachimbaji wetu wanataka watengenezewe mazingira bora ya uchimbaji, kwa sababu hali iliyoko pale siyo nzuri, na siyo kuwahamisha: Ni lini sasa mtawapatia mikopo wachimbaji wa Kinyambwiga na Gwishigwamara ili waweze kununua mashine ya kisasa na waweze kuchimba kama wachimbaji wengine kwenye maeneo mengine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Answer

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubali kwamba Kinyambwiga na maeneo mengine aliyoyataja ni maeneo ambayo kwenye Wilaya ya Bunda ndiyo yanatupatia mapato mengi sana. Wachimbaji wa kule wanafanya kazi nzuri ya kuchimba. Pamoja na kwamba kuna changamoto kidogo za ki-management, katika eneo lile wako watu ambao wana mashamba, wako watu wenye leseni, tunakamilisha ule mgogoro ili uchimbaji uendelee kufanyika kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo, ni kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, ni lazima tukubali Waheshimiwa Wabunge kwamba, kumpatia mtu fedha ni lazima kuwe na utaratibu ambao uta-guarantee fedha hiyo kuweza kurudi na kuwakopesha watu wengine. Tusingependa kutoa mikopo ambayo mwisho wa siku fedha hizi zitapotea na aliyepewa pesa haonekani na pesa hazionekani na tunashindwa kuwakopesha wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungeomba Waheshimiwa Wabunge watupe muda, study hii inaendelea na Mheshimiwa Rais mwenyewe analijua jambo hili na ametupa maelekezo mahususi ya kuangalia namna bora ya kulifanyia kazi ili wachimbaji wetu waweze kupata tija.

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo katika Wilaya ya Mbogwe?

Supplementary Question 4

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema kuna uchimbaji wa wachimbaji wadogo kwenye maeneo ya leseni, na kuna wachimbaji ambao wanachimba kwenye eneo la rashi; lakini wachimbaji hao wadogo wanatumia fedha na gharama kubwa kutoa ile mifuko ndani ya ardhi. Unakuta anatoa mifuko 100, lakini wasimamizi wa kwenye rashi wanachukua asilimia 40: Kwa kuwa wao husimamia tu: Serikali inatoa kauli gani ili kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo, ipunguze hiyo mifuko 40? (Makofi)

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Answer

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati njema Mheshimiwa Amar ni mchimbaji mzoefu na anajua sekta hii. Tulikotoka ilikuwa mchimbaji mdogo anachimba anatoa mawe, msimamizi au miaka ile walikuwa wanaitwa ma-digger, yeye peke yake anachukua asilimia 70. Serikali tulitoa mwongozo maalum wa usimamizi wa rash na tukasema hivi, katika uchimbaji wowote unaofanyika mahali popote kwenye maeneo yasiyokuwa rasmi, mgawanyo utakuwa kama ifuatavyo: asilimia 15 itakwenda kwa mwenye shamba, asilimia 15 itakwenda kwa msimamizi, na msimamizi fedha hiyo atakayoipata itatumika kwa ajili ya kujenga miundombinu kama vile vyoo na huduma mbalimbali maeneo ya uchimbaji huo. Asilimia 70 yote inayobaki ni kwa ajili ya mchimbaji ambaye yuko kwenye shimo anayetumia nguvu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu ni huo na mwongozo upo. Kama kuna mahali unakiukwa, tuwasiliane Mheshimiwa Mbunge ili tuchukue hatua. (Makofi)