Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Bunju B – Mabwepande – Kibamba utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, majibu yanaonesha kwamba usanifu utakamilika mwezi Machi, 2024. Sasa kwa kuzingatia umuhimu wa hii barabara ina hospitali kubwa ya Mabwepande ambayo kama wagonjwa wakizidiwa pale wanapelekwa referral Hospitali ya Mloganzila.

Sasa nataka commitment ya Serikali kwamba kwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025 kwa sababu usanifu utakuwa umekamilika je, fedha zitaanza kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii? Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, kuna barabara ya Old Bagamayo ambayo inaanzia Morocco, Mwai Kibaki, Daraja la Mlalakuwa pale, Kawe Round About mpaka Afrikana; hii imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana ya upanuzi wa ile barabara, na kuna foleni kubwa sana pale, nataka vilevile kupata commitment ya Serikali kuwa ni lini upanuzi wa ile barabara utafanyika ili kupunguza kero ya foleni kwa wananchi?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba hii barabara ya Bunju B – Mabwepande hadi Kibamba ni barabara muhimu sana na imekuwa ikiulizwa mara kwa mara hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge ambao barabara hiyo inapita kwao akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo ambapo wiki iliyopita niliulizwa swali hili.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sio tu tunafanya usanifu wa kujenga barabara kama ya barabara ya kawaida kama alivyosema tunajua kuna hospitali, lakini pia tunajua barabara hii kwa sababu pia kuna Kituo cha Mabasi cha Magufuli kitatumika kwa umakini mkubwa sana itakapojengwa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, barabara hii nataka nimjulishe Mheshimiwa Mbunge si tu kwamba itaishia hapo lakini ita–save kama barabara ya mzunguko wa nje kwa Dar es Salaam ambayo itatoka hapo Kinamba – Pugu – Toangoma hadi Kigamboni ndio maana huu muda umekuwa mrefu. Kwa hiyo, hako kaeneo alikouliza ni sehemu tu ya hiyo barabara.

Kwa hiyo, commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara hii tunaijenga kwa sababu sasa tunajua umuhimu wake ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hizi barabara alizosema za kufanya upanuzi kwa sababu ya misongamano, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara alizozitaja tumeziainisha vizuri sana katika kitabu chetu cha bajeti barabara zote za kupunguza misongamano ikiwa ni pamoja na kupanua. Katika kitabu chetu cha bajeti cha mwaka huu barabara nyingi za Dar es Salaam tutazipanua ambazo zinapatikana katika ukurasa wa 259 – 261 atazikuta hizi barabara zote na nini tunafanya katika mwaka huu huu wa fedha ambao tunauendea wa 2023/2024, ahsante sana.

Name

Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Primary Question

MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Bunju B – Mabwepande – Kibamba utaanza?

Supplementary Question 2

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniruhusu niulize swali moja la nyongeza.

Ni lini Serikali itajenga barabara ya mwendokasi yaani BRT - 4 ambayo kipande kikubwa kinaanzia Mwenge - Makongo Sekondari, Lugalo Jeshini, Mbezi Beach, Tegeta kwa Ndevu, Nyaishozi mpaka Basihaya ambayo pia itaondoa mafuriko yanayoikumba Basihaya kwa kujenga mitaro? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nataka nimjulishe Mheshimiwa Mbunge wa Kawe kwamba barabara aliyoitaja iko kwenye BRT - 4 ambayo itaanzia Maktaba itakuja Mwenge mpaka pale Daraja la Kijazi hiyo itakuwa ni Lot ya kwanza; na Lot ya pili itaanzia Mwenge – Tegeta mpaka kuja huku DAWASA.

Kwa hiyo, tutakuwa na wakandarasi wawili; lot ya kwanza ndiyo hiyo na lot ya tatu itakuwa ni mkandarasi ambaye atajenga majengo.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tarehe 30 Juni, 2023 siku ya Ijumaa pale DAWASA tunakwenda kusaini mikataba hiyo ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo ya BRT - 4, ahsante sana. (Makofi)