Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Primary Question

MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:- Je, lini Serikali itawapa ajira za kudumu walimu walioajiriwa tangu mwaka 2002 kwa masharti ya ajira za muda Ulyankulu?

Supplementary Question 1

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuishukuru Serikali kwa hatua iliyofikia kuhusu hawa walimu wangu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na Serikali kutuambia kwamba hawa walimu 13 ambao walikuwa ni raia wa Burundi, wakimbizi, wamepatiwa ajira, lakini mpaka tunavyoongea hivi, hakuna barua waliyopewa inayoonesha kwamba wamepewa ajira za kudumu: Je, Serikali iko tayari kuiambia Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua na mamlaka zinazoshughulikia masuala ya walimu kuhakikisha hawa walimu wanapata barua zao za ajira na stahiki nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kuna walimu hawa 29 ambao umri wao umevuka miaka 45 walikuwa wanajazishwa mikataba ya muda, lakini pamoja na kujazishwa mikataba ya muda walikuwa hawapewi gratuity yao.

Je, pamoja na kwamba wamejazishwa hii mikataba, lini watapewa stahiki zao kulingana na mikataba waliyokuwa wamejaza? Ahsante. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la kwanza la Mheshimiwa Migilla la hawa 13 kwamba bado hawajapata barua za ajira zao, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge na kuwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kaliua na kuona changamoto iko wapi kwa ajili ya hao walimu kupata barua zao kama ambavyo kibali kilitolewa na Ofisi ya Rais, Utumishi kwa ajili ya kuweza kuwaingiza katika ajira ya kudumu.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, hili ni suala la kisheria. Ni sheria iliyopitishwa na Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, mtumishi yeyote wa umma ni lazima anapoingia katika utumishi wa umma asiwe amevuka umri wa miaka 45 ili aweze kuwa amechangia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa miaka isiyopungua 15. Ndiyo maana hawa baada ya kupata uraia wao na vibali kutoka Ofisi ya Rais, Utumishi walikuwa wameshavuka ule umri wa miaka 45.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, Katibu Mkuu Utumishi alitoa kibali kwa hawa 29 kuendelea kuwa na ajira ya mkataba, ambapo ni mikataba ya miaka mitano mitano, tofauti na mikataba mingine ya mwaka mmoja mmoja. Watapata kiinua mgongo chao pale watakapofikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ilivyo ya kustaafu.