Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saumu Heri Sakala

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SAUMU H. SAKALA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi yake ya kuanza kuwalipa wazee pensheni?

Supplementary Question 1

MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Suala hili la wazee kulipwa pensheni kila siku limekuwa likitajwa, lakini nashangaa kidogo nikisikia bado hata hayo maandalizi hayajaanza. Je, Serikali inaweza kusema nini kinakwamisha maandalizi hayo ambayo mpaka sasa hayajaanza na kwa kutambua umuhimu huo wa wazee?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, maandalizi hayo yataanza lini na yatamalizika lini? Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Saumu Heri Sakala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza limeuliza ni nini kinakwamisha. Kwanza kabisa nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina dhamira njema kabisa ya kuhakikisha inatekeleza ahadi yake ya kuwalipa pensheni wazee kwa kutambua mchango mkubwa ambao wazee wameutoa katika Taifa hili katika sekta za huduma za jamii, kiuchumi na kisiasa. Kwa hiyo, Serikali inatambua kabisa umuhimu wa wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kinachokwamisha hapa si kwamba kuna jambo ambalo linakwama, lakini mipango ya Serikali ilikuwa kwanza kuhakikisha inatengeneza miundombinu ambayo ndiyo itakwenda kulifanya jambo hili liwe endelevu. Kwa hiyo, katika uratibu wa zoezi zima, awali ilikuwa ni kutayarisha mpango rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mpango huu unaanza kufanyiwa kazi na tayari mpango huu umekamilika zimebaki hatua chache tu za kuona ni namna gani mpango huu utaanza sasa kutekelezwa pale ambapo mamlaka husika zitahusishwa na fedha zitakuwa zimepatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza ni lini itaanza. Nirudie tu katika jibu langu la msingi kwamba zoezi hili ni kubwa sana ambalo linahitaji umakini mkubwa sana na lengo la Serikali ni kulifanya kuwa endelevu. Hata katika baadhi ya nchi ambazo wamefanya zoezi hili kwanza kabisa walifanya namna ambavyo ilikuwa inawapa picha waanzaje ndiyo baadaye waje walikamilishe kwa uzito wake. Kwa hiyo, na sisi kwa kutambua kwamba jambo hili ni kubwa na linahitaji rasilimali fedha, Serikali imeanza kwanza na ujenzi wa miundombinu ya kuratibu zoezi zima ili baadaye kuweza kuwafikia wazee hawa kwa maana ya kuwalipa pensheni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufuatilia jambo hili tulikwenda kujifunza katika baadhi ya nchi ambazo zimefanikiwa sana. Ukienda kule Nepal ambao ni kati ya watu waliofanikiwa, wana kitu wanakiita Nepal’s Senior Citizens’ Allowance na wenyewe walianza katika utaratibu huu huu. Walianza kwanza kuwalipa wazee kuanzia umri wa miaka 60 lakini baadaye wakaona namna gani waweze kuingiza na makundi mengine. Kwa hiyo, na sisi tunatafakari mpango huu mzima lengo letu ni kuufanya mpango huu uwe endelevu.

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. SAUMU H. SAKALA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi yake ya kuanza kuwalipa wazee pensheni?

Supplementary Question 2

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza mimi nasikitika kwa sababu Serikali inaonekana haina nia njema juu ya jambo hili. Mimi nikiwa Mbunge mwaka 2004 Serikali ilitoa majibu haya haya, mwaka 2008 Serikali ikatoa majibu haya haya, mwaka 2012 Serikali ikatoa majibu haya haya. Mimi ni Mbunge kwa kipindi cha nne sasa, nasikitika sana juu ya majibu yenu ambayo … (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa swali kwa ufupi naomba tafadhali.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni moja tu, uzee na kuzeeka nani ataukwepa, hakuna na kila mmoja ni mzee mtarajiwa. Serikali ituambie sasa ina mkakati gani wa ziada na kama mlivyosema kuwa hatua chache zimebakia, hizo hatua chache ni zipi? Je, ndani ya miezi mitatu mnaweza kumaliza suala hili ili wazee wapate pensheni zao hasa ukizingatia na wale baadhi waliopigana Vita vya Kagera?

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, lakini nikiendelea kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya dhati ya jambo hili na ndiyo maana katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 jambo hili limewekwa na kutafsiriwa vizuri sana. Kipindi cha nyuma jambo hili halikuwa limechukua picha ya kutosha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Hiyo tu kwanza ni nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha jambo hili linatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ameeleza vizuri sana na naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba suala hili sio la kulala na kuamka ndani ya miezi mitatu halafu ukasema unaanza tu kulipa pensheni, hapana.
Narudia kusema Serikali imeshaanza kutengeneza miundombinu ya kulifanya jambo hili liweze kutekelezeka.
Sheria inayompa mamlaka Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kifungu cha 5(1)(e), kimemuagiza na kumwelekeza Mdhibiti kuhakikisha anasimamia suala zima la kuona namna gani Watanzania wengi wanafikiwa na sekta ya hifadhi ya jamii ikiwemo wazee.
Kwa hiyo, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu Serikali inalifanyia kazi suala hili na mara litakapokamilika litaanza kuchukua nafasi yake na wazee watapata pensheni.