Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?

Supplementary Question 1

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ahadi hii sasa ina miaka Sita na inaenda mwaka wa Saba, ahadi zote zinazotolewa na Viongozi wetu wa Kitaifa wanatoa kwa sababu ya hali ilivyo ngumu kwenye Majimbo yetu yaliyo mengi. Ninavyojua kwa Viongozi wa Kitaifa ni sehemu ya maelekezo ya Serikali, ahadi hii hata hayati marehemu John Kwandikwa aliifuatilia sana lakini utekelezaji wake mpaka leo haujafanyika.

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ahadi hii na kwa nini Serikali isitafute fedha za ziada kuhakikisha kituo cha afya hiki kinajengwa?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichoeleza ni kwamba hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nieleze tu Bunge lako tukufu kwamba moja ya mpango mkubwa wa Serikali ambao ulikuwepo awali ni kuhakikisha kwamba zile Tarafa zote nchini ambazo hazikuwa na vituo vya afya tulikuwa tunapeleka vituo vya afya, ndiyo maana katika mwaka wa fedha huu unaokwenda kuisha Serikali imepeleka fedha za ujenzi wa vituo vya afya 233 ikiwemo katika Jimbo la Ushetu ambapo tumepeleka fedha awamu ya kwanza, fedha za tozo Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho wao wamepeleka katika eneo lingine.

Meshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika eneo hili ambalo liko katika ahadi baada ya kumaliza huu mkakati ambao tumeuainisha kumaliza Tarafa zote nchini basi na eneo lako tutaliweka katika kipaumbele kuhakikisha kwamba hii ahadi haichukui muda mrefu ili kuwasaidia wananchi wa Kata ya Ulowa. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?

Supplementary Question 2

MHE. EMMANUEL E. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Tabora Mjini wananchi kwa nguvu zao wamejitahidi sana kujenga vituo vya afya ambavyo vingi viko kwenye maboma lakini wengine wamekusanya mawe na kujitolea nguvu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kusaidia kumalizika kwa hivi vituo vya afya ambavyo wananchi wamejitoa nguvu zao?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatambua maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Tabora Mjini wananchi wameshiriki kwa nguvu zao kuchangia ujenzi wa vituo vya afya na maboma yako mengi karibu kila Mbunge hapa anaweza kuyaainisha. Kwa hiyo, wakati wa sasa ukiwa ni mpango wa kuhakikisha kwamba Halmashauri zote zinapata hospitali za Wilaya, ambapo tulikuwa na Halmashauri 28 hazikuwa na hospitali za Halmashauri ambapo mwaka huu wa fedha Serikali imepeleka fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa pili ilikuwa ni kumaliza Tarafa zote nchini, tulikuwa na Tarafa 570, karibu Tarafa 233 zilikuwa hazina ambapo Serikali tumepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa maeneo hayo. Kwa hiyo, mpango wa tatu utakuwa sasa ni kwenda kumalizia katika yale maeneo ambayo wananchi wameweka nguvu zao. Kwa hiyo, haya masuala ni yanakwenda kwa mipango na kwa muda kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalitambua hilo na tutatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapeleka fedha ku-support wananchi nguvu zao walizozitoa. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?

Supplementary Question 3

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza kwamba Tarafa ya Matamba kuna kituo cha afya cha Matamba kina takribani miaka 30, hakina jengo la Mama na Mtoto na wala hakina jengo la mochwari. Huduma ya mochwari tunaenda kupata kwenye Wilaya ya jirani inaitwa Chimala. Sasa tunaomba ni lini Serikali itatupatia fedha tuweze kujenga jingo la mama na mtoto lakini eneo la kuhifadhia wenzetu kwa maana ya mochwari, kwa sababu ni umbali mrefu tunaenda kuhudumiwa kutoka kwa Jirani?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameainisha kwamba Tarafa ya Matamba ina kituo cha afya lakini hakina huduma ya mochwari pamoja na mama na mtoto, kwa hiyo alichoomba tu ni kwamba Serikali lini tutapeleka fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu kwamba tumelipokea hili ombi na tutaliweka katika mipango yetu ya baadaye ili tuhakikishe kwamba hizi huduma mbili ambazo ameziainisha Mheshimiwa Mbunge zinapatikana. Ahsante. (Makofi)

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?

Supplementary Question 4

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango ambayo Serikali imeainisha hapa ya ujenzi ya vituo vya afya lakini hakuna mpango wa wazi wa kuonesha namna gani sasa tunajenga vituo vya afya lakini tunaajiri watumishi wa sekta ya afya tukizingatia kwamba tuna upungufu wa takribani asilimia 50 ya watumishi wa afya kwenye sekta zetu za afya? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inajenga na moja ya mkakati tulionao ni kuajiri na hata katika mwaka huu wa fedha nafikiri kama wiki ijayo Mheshimiwa Waziri wa Nchi atatangaza nafasi za ajira ambazo tutakwenda kuajiri katika maeneo haya ya afya pamoja na elimu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali imejipanga kuajiri na Waziri wa Nchi atatangaza hilo. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?

Supplementary Question 5

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni Mashariki tuna Kituo cha Afya cha Kintiku ambacho tayari Serikali ilishajenga jengo la maabara, jengo la x-ray, wodi ya mama na mtoto na mochwari, lakini hatuna jengo la OPD. Ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba wanatupatia jengo la OPD?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Chaya Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameainisha kwamba katika Kituo cha Afya cha Kintiku kinachokosa tu ni jengo la OPD na nimhakikishie tu kwamba maeneo yote ambayo yana mapungufu na sisi tulipeleka fedha tutamaliza majengo, kwa sababu maeneo mengine yanakosa mochwari, maeneo mengine yanakosa maabara, mengine yanakosa wodi za akina mama, kwa hiyo lipo katika mpango ikiwemo katika eneo hili la Kintiku ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliainisha. Ahsante.

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?

Supplementary Question 6

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika Kituo cha Afya cha Ukuge ulijengwa mtambo mkubwa uliokusudiwa kutengeneza oxygen kwa ajili ya Kanda yote ya Magharibi, lakini bahati mbaya mtambo ulipowashwa, ukawa unatengeneza nitrogen.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuchukua mpango huo unaotengeza nitrogen ili watuletee unaotengeneza oxygen?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichokielezea kuhusu huo mtambo ili Serikali ichukue najua suala hili linahusu zaidi Wizara ya Afya. Kwa hiyo, kwa niaba ya Wizara ya Afya, tuseme tumelipokea hilo na Serikali italifanyia kazi. Ahsante sana.