Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, ni fursa zipi anazopata Askari anayeoa au kuolewa na Askari mwenzake?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka mingi sasa toka ukoloni vijana wetu wanaoajiriwa na Jeshi la Kujenga Taifa wanapewa miaka Sita kabla ya kuolewa au kuoa. Kwa kuwa, magonjwa yamekuwa mengi na kwa kuwa stress za Askari wetu zimekuwa nyingi.

Je, ni lini Serikali itapunguza muda huu wa miaka Sita kuwa miaka Mitatu au Miwil?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni muda sasa tunapeleka vijana wetu JKT tunapeleka vijana 2,000 au 1,000 wanachukuliwa labda 50 wanaajiriwa wengine wanarudi nyumbani. Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango mkakati wa kuandaa vijana wanaorudi nyumbani kuwapa ufundi wa kutosha na saikolojia ili wasiwe panya road? (Makofi)

Name

Dr. Stergomena Lawrence Tax

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Getere kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaanza kwa kumpongeza kwa kuwa mdau wa karibu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kuwatetea wapiganaji wetu. Swali lake la kwanza ambalo ni kuhusu umri, napenda kwanza nitoe ufafanuzi kwamba ni kweli kwamba Maafisa na Maaskari wenye elimu ya darasa la saba hadi kidato cha sita na wenye Stashahada wao ndiyo hukaa miaka Sita kabla ya kuolewa. Yapo makundi mengine kama wenye shahada ya kwanza wao hukaa kama makapera kwa miaka Minne na wenye Shahada ya Uzamili, wao hukaa kwa miaka mitatu na wenye Shahada ya Uzamivu wenyewe hawana muda wa kukaa kwenye ukapera na hii ni kutokana na aina ya majukumu ambayo maaskari hawa wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Askari ambao nimewataja katika kundi la kwanza hao huwa ni vijana wadodo wanajiunga wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, kwa hiyo huhitaji kwanza kukomaa. Majukumu ya Jeshi ni majukumu mahususi lakini pia hawa ndiyo wanategemewa kama wapiganaji kwa hiyo huendelea na kozi mbalimbali na kuhakikisha kwamba wako imara wakati wote. Kwa hiyo, miaka hii Sita iliyowekwa imewekwa baada ya kufanya uchunguzi lakini pia kuzingatia vigezo mbalimbali. Kwa hiyo, kama tunaweza kubadilisha sidhani kama hilo linawezekana kwa sasa kwa sababu utafiti ulifanyika na lazima iwe hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii pia inatokana na aina ya majukumu ambayo wanafanya. Wengine wanapoajiriwa kama Madaktari huenda moja kwa moja kufanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo linahusiana na vijana wanaokwenda JKT kwamba ni wengi lakini wanaoajiriwa ni wachache. Kwanza ninapenda kueleza kwamba madhumuni ya vijana kujiunga na JKT ni kuwajengea uzalendo, kuwajengea ukakamamu lakini kuwapa stadi mbalimbali ili baada ya hapo waende kujiajiri. Madhumuni siyo kutoa ajira kwa vijana hawa, hilo linafanyika vijana hawa wanafundishwa stadi mbalimbali ili baada ya hapo waweze kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tuna mpango gani, ni kweli nasi tumeona kwamba pamoja na kuwapa stadi mbalimbali bado kuna umuhimu kuwawezesha vijana hawa kujitegemea. Kwa hiyo, tumeanza kufanya kazi hii na tayari katika mpango wa block farming kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, tutaona jinsi gani tutaweza kuchukua baadhi ya vijana, lakini bado tunaendelea kulichakata suala hili tuweze kuja na program nzuri zaidi ambazo zitawawezesha vijana hawa kujiajiri baada ya kupata stadi ambazo tunawapatia. (Makofi)