Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:- Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora inakabiliwa na kero mbalimbali kama vile ukosefu wa madaktari bingwa wa watoto, akina mama, mifupa, na kadhalika; ukosefu wa vifaa muhimu kama vile ECG machine, CT-Scan, MRI machine, ukosefu wa huduma za ICU pamoja na kwamba lipo jengo zuri lakini halina vifaa vya huduma za dharura:- Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutatua kero hizi zinazokabili hospitali hii kwa muda mrefu?

Supplementary Question 1

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii niweze kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kuipongeza Serikali kwa kutupelekea madaktari wawili kwenda kusoma waje kuwa Madaktari Bingwa kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kutusaidia sisi ambao tuko mikoa ya pembezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wale ma-volunteer wa Kichina watano anaosema ni Madaktari Bingwa, wanaingia hospitali saa 5.00 na kutoka saa 7.00. Kwa maana hiyo, hawatusaidii ile ni Hospitali ya Rufaa, wagonjwa wanaingia ndani ya masaa 24. Kwa hiyo, wale Madaktari wa Kichina watano anaowasema hawatusaidii ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikisema Bungeni hapa toka 2011 nikidai Madaktari Bingwa wa Mkoa wa Tabora, akina mama wanapata vifo vingi vya uzazi, watoto wetu wanakufa kwa sababu hatuna Madaktari Bingwa, vijana wetu madereva wa bodaboda wanavunjika miguu, hatuna Madaktari Bingwa wa Mifupa. Hii imekuwa kero kubwa kwetu sisi Wabunge ndani ya Mkoa wa Tabora na nimekuwa nikilisemea hilo kwa muda mrefu toka 2011 naingia hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri hajanijibu vizuri, ana mkakati gani wa kutuletea Madaktari Bingwa ndani ya Mkoa wa Tabora?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba vibali miaka 10 iliyopita lakini hatujapewa kibali cha kuajiri Madaktari hao. Naomba anijibu ana mkakati gani wa kutuletea Madaktari Bingwa katika Mkoa wa Tabora kwa sababu watu wanakufa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na vifaa. Niipongeze Serikali kwa mkakati wake mzuri wa kusema kwamba Bima ya Afya itatukopesha na tupate vifaa ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Hospitali ni ya siku nyingi, haina vifaa vyovyote, watu wanaendelea kufa. Hata hivyo, nimesema hatuna huduma ya ICU pale Tabora…
Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kufuatana nami kwenda Tabora kuangalia changamoto zilizopo katika Hospitali ya Rufaa?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, usimuone Mheshimiwa Munde ana-rap sana ni kwamba ameguswa na jambo hilo na ndiyo maana nimesema kwamba Serikali imepeleka madaktari kwa ajili ya kwenda kubobea katika maeneo hayo na lengo kubwa na mahsusi ni kwa ajili ya Mkoa wa Tabora, hili ni jambo moja kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafahamu fika, wiki chache zilizopita nilifika Mkoani Tabora pale. Nilienda katika Kituo cha Afya cha Bukene na Itobo, kote kuna vifaa vya upasuaji vinataka wataalam. Hata katika kipaumbele chetu tumesema suala la Mkoa wa Tabora lazima liwe kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana wataalam wetu, mara nyingi sana hospitali zilizoko pembeni madaktari wanaona ni tabu sana kwenda kwenye maeneo hayo. Sisi sasa hivi tumejipanga, lengo letu ni kuelekeza wataalam kwenye maeneo yote ya pembezoni na kuhakikisha kwamba wataalam wanaosomeshwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaenda kuwahudumia Watanzania.
Suala la vifaa nimesema pale mwanzo na Waziri wa Afya na yeye analizungumza mara nyingi sana kwamba suala la vifaa kuna utaratibu maalum. Naomba niwaambie, kuna mchakato mkubwa sana wa hivi vifaa mwisho wa siku Hospitali zote za Kanda na Mikoa zifungiwe vifaa maalum ili mradi akina mama na wagonjwa mbalimbali waweze kuhudumiwa. Huu ni mpango mkakati wa Serikali na unaanza mwaka huu. Kwa hiyo, dada yangu Munde usihofu, mimi mtani wako umesema tuongozane, nitaongozana na wewe Mungu akijalia. (Makofi/Kicheko)


WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi (TAMISEMI), napenda kuongeza kidogo ufafanuzi katika suala la uhaba wa watumishi especially Madaktari Bingwa, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tumefanya tathmini ya uhaba wa watumishi katika sekta ya afya, especially Madaktari na Madaktari Bingwa. Tumebaini mikoa tisa ina uhaba mkubwa ikiwemo Tabora, Simiyu, Katavi, Geita, Shinyanga, Rukwa na Singida.
Kwa hiyo, kipaumbele cha ajira za Madaktari Bingwa katika mwaka huu tunatoa katika mikoa hiyo tisa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Munde na Waheshimiwa Wabunge wengine wote ambao mnatoka katika hiyo mikoa tisa tutawapa kipaumbele kwa sababu mnao uhaba wa wataalam chini ya 52%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumekusudia kufanya zoezi moja kugumu sana. Tunataka kuondoa tatizo la Madaktari Bingwa wataalam kurundikana katika mkoa mmoja na kuiacha mikoa ya pembezoni, kwa hiyo, tunataka kuangalia mgawanyo.
Waheshimiwa Wabunge mtuvumilie tutakapoendesha zoezi hili gumu mkasema huyu naomba umbakize, mwanamke wa Rukwa, Katavi, Njombe, Simiyu, ana haki ya kupata huduma za Daktari Bingwa kama mwanamke wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunataka kuendesha zoezi la redistribution, tuwatawanye madaktari waende mikoani wakatoe huduma ili wanawake wa huko wapate huduma nzuri kama wanawake wa Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)

Name

Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:- Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora inakabiliwa na kero mbalimbali kama vile ukosefu wa madaktari bingwa wa watoto, akina mama, mifupa, na kadhalika; ukosefu wa vifaa muhimu kama vile ECG machine, CT-Scan, MRI machine, ukosefu wa huduma za ICU pamoja na kwamba lipo jengo zuri lakini halina vifaa vya huduma za dharura:- Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutatua kero hizi zinazokabili hospitali hii kwa muda mrefu?

Supplementary Question 2

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Kwa kuwa matatizo ya ukosefu wa huduma katika Hospitali za Mkoa wa Morogoro hayana tofauti na matatizo ya Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Morogoro una Hospitali ya Rufaa ambayo inatoa huduma katika wilaya zake zote lakini cha kusikitisha hospitali hiyo haina huduma ya X-ray. Huduma ya X-ray iliyopo ni ya zaidi ya miaka 20 iliyopita hali ambayo inawalazimu wagonjwa waliolazwa hata wodini kwenda kupata huduma za X-ray nje ya hospitali hiyo katika Hospitali za Mzinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapeleka huduma hizo za X-ray katika Hospitali hii muhimu ya Rufaa ambayo inategemewa na wananchi wa Mkoa wa Morogoro?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, hiki kilio tumekisikia na tunajua Morogoro ni center. Ukisema huduma ya X-ray pale Morogoro hakuna wakati tukijua Morogoro ni muungano wa barabara mbili, inayotokea Dodoma na ile inayotokea Iringa, na katika njia moja au nyingine kama kesi za ajali za magari lazima mgonjwa moja kwa moja atapelekwa katika Hospitali ya Mkoa. Sasa kama changamoto hii ni kubwa kiasi hiki, naomba niseme katika zoezi letu la kupeleka vifaa vya upimaji tutahakikisha Morogoro inapewa kipaumbele. Naomba aiamini Serikali yake itaenda kufanya kazi hiyo haraka iwezekanavyo.