Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuwawezesha Wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana ajira kulipa mikopo yao?

Supplementary Question 1

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa jawabu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya wahitimu ambao wanashindwa kupata kazi au kujiajiri wanaamua kuondoka nchini kwenda nchi za nje kufanya kazi na wakati huo mkopo wao huku hawajalipa; ingawa kuna wazazi au wadhamini wanaambiwa wao wausimamie mkopo huo, mzazi huyu ni masikini, hana uwezo wala hajui ataipata wapi hiyo pesa: Je, deni hili hitalipika vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa baadhi ya wahitimu wako mitaani, hawana kazi, hawawezi kujiajiri na ambao elimu yao ni ya juu; na vile vile wahitimu hao wanapokuwa mitaani wanaweza kufanya mambo ambayo siyo mazuri kisheria, ingawa wao wanasema wanawapa elimu, kuna mkopo wa asilimia 10, wengine wajasiliamali.

Kwa nini wasingewakusanya wakawafundisha kazi za kujitegemea ambazo wazee wetu walikuwa wanafanya, kama upishi wa kitaalam, ufundi wa ujenzi, ufundi mchundo ila ni wa kitaalam kulingana na elimu yao waliyonayo na wakimaliza kuwapatia kitu kidogo ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamis kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye eneo la kwanza la wahitimu ambao wanamaliza na kwenda nje ya nchi kufanya kazi na huku wakiacha deni katika bodi yetu ya mkopo, kumekuwa na utaratibu mzuri wa Serikali kwa sasa wa kuendelea kuratibu watu ambao wako nje ya nchi (diaspora) wakiwa wanafanya kazi huko na kuweza kutengeneza arrangement za kuweza kuwafanya wao yale madeni yao yaweze kulipwa. Taarifa hizi tumekuwa tunazipata kutoka upande wa wadhamini wao ambao wanabaki hapa nchini. Kwa hiyo, suala hili tunaendelea kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwemyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa kwa kuliona na kuendelea kuwa mfuatiliaji ili fedha hizi zisipotee ambazo tunatarajia ziwasaidie vijana walio wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameuliza pia kuhusu wahitimu walio mtaani, kama kuna mpango wowote wa Serikali wa kuwasaidia. Tayari vijana wapo ambao wamechukuliwa na vyuo mbalimbali. Tunavyo Vyuo vya VETA ambavyo vinatoa mafunzo hata sasa. Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi bilioni tisa kwa kuwasaidia vijana zaidi ya 14,432 katika Vyuo 72 vya VETA hapa nchini na tayari wanaeleleka kuhitimu katika awamu ya kwanza katika miezi sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa sasa ukiangalia katika upande wa Wakala wa Ajira (TaESA) kumekuwa na utaratibu huo wa kuwasaidia vijana kupata ajira na pia kupata mafunzo ya namna ya kuomba kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, pia tumeingia katika mpango mwingine mpya. Sasa hivi tunafanya study ya kuangalia nchi nyingine ambazo zina changamoto kubwa ya masuala ya ajira na tunafanya study China, Marekani, Uswiss, Ubeligiji, Ufaransa, Rwanda, Burundi na Kenya ili tuweze kuangalia wenzetu kwenye eneo la ajira wamefanya kwa kiwango gani. Hivi karibuni nitatoa taarifa ya kuhusiana na changamoto za ajira jinsi nchi nyingine ambavyo wameendelea kuzikabili. Ahsante.

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuwawezesha Wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana ajira kulipa mikopo yao?

Supplementary Question 2

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa majibu ya Serikali, siku zote yamekuwa yakiamini kwamba tatizo la ajira la vijana litatatuliwa kwa kutegemea Serikali Kuu ama public sector. Sasa ni wazi kwamba Serikali inatoa ajira kwa 2% tu ya mahitaji yote ya ajira. Huo ndiyo ukweli. Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza kwamba changamoto ni private sector ya nchi hii iko duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limekuwa likielezwa kwenye taarifa zote za Mipango ya Miaka Mitano ya Serikali; 2011, 2015, 2015/2020 kwamba Sekta binafsi ya nchi hii inafanya vibaya. Sasa niiulize Serikali: -

Je, mna mikakati gani na mmekwama wapi mpaka miaka 10 ya Mipango ya Maendeleo ya nchi hii? Mnaonekana mmefeli kabisa kusaidia sekta binafsi ichanue. Kwa sababu ikichanua ndiyo vijana wetu watapata ajira kwenye maeneo mengine. Mmekwama wapi? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee ambaye anauliza tumekwama wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie kwamba Serikali haijakwama popote. Mkakati wa kwanza ambao tumeufanya kama Serikali ni kufanya mapitio yote ya sera katika sekta binafsi ili kuweza kuziboresha zaidi na kuendana na uhitaji wa kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tumechukua hatua pia katika kubadilisha sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uwekezaji ikiwemo Sheria ya Kuratibu ajira za wageni ambapo sasa tumebadilisha na kuruhusu watu ambao wanahitaji kuja kuwekeza nchini, kupunguza yale masharti yaliyokuwepo hapo awali; na unaweza ukaona kuanzia hivi sasa hata kufikia yale mapato yanayopatikana kwa kuomba vibali vya kazi, imefikia zaidi ya bilioni 145. Kwa hiyo, hiyo ni hatua kubwa ambayo Serikali Awamu ya Sita inafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine, ipo pia mikakati ya kuandaa maeneo maalum ambayo ni maelekezo katika maeneo ya kuongeza fursa za ajira kwa vijana. Ni agizo la Mheshimiwa Rais kwamba katika kila Wizara ya Kisekta kwenye mwaka wa bajeti itakapotengewa fedha, ile bajeti katika matumizi yake ilete implication ya ajira ngapi zitapatikana kutokana na fedha hizo ambazo zimetolewa katika mwaka wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la nne ni hilo la kimkakati ambao tumeendelea kufanya utafiti katika nchi nyingine. Suala la ajira ni mtambuka na liko ulimwenguni kote. Nitolee mfano China, wana population ya bilioni 1.3, lakini katika population hiyo ya 1.3, tatizo la ajira walikuwa wameli- address kwa asilimia 64 tu. Katika asilimia 40 katika kila mwaka unaoingia kunakuwa kuna immigrants wanaoenda kutafuta ajira kutoka nchi ya China, population zaidi ya watu milioni 150.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna hatua mbalimbali ambazo wamezichukua na tunafurahishwa kwamba ukisoma hizi ripoti na taarifa, hata ile ya International Labor Organization, inaonyesha kwamba Tanzania tumepiga hatua na tumeenda katika mikakati mizuri ya kutatua tatizo la ajira. Ahsante.