Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: - Je, ni upi mgawanyo wa vitabu 812 vya nukta nundu vilivyotolewa katika Mpango wa Fedha za Mapambano dhidi ya UVIKO 19?

Supplementary Question 1

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba niipongeze Serikali kwa majibu mazuri na wameonesha kabisa kwamba mmeongeza vitabu. Pamoja na hayo yote naomba niongeze swali la kuhusu watu wenye uoni hafifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye uoni hafifu shuleni wanapata taabu sana, kwa sababu Walimu wengi hawafahamu namna ya kuwafundisha hawa watu ili waweze kuelewa. Wanapata tabu ubaoni na kwenye karatasi kwa sababu maandishi yanakuwa ni madogo. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka mwongozo kwenye shule zote na Walimu wote wafahamu namna gani ya kuwafundisha watoto wenye mahitaji maalum, hasa hao wenye uoni hafifu ambao wengi ni wenye ulemavu wa ngozi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tunafahamu kabisa, katika suala la afya na maradhi watu wenye ulemavu wanapata shida sana na wanapata maradhi kutokana na hali ya usafi na mazingira pale shuleni. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha miundombinu, kuongeza vyoo vya watu wenye ulemavu shuleni ili hawa watu waweze kusoma vizuri? Kwa sababu tunaamini kabisa kwamba elimu ndio ufunguo wa maisha na elimu ndiyo mkombozi wa watu wote wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khadija taya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anayoyazungumza Mheshimiwa, kwamba wenzetu wenye uoni hafifu, hasa wenzetu wenye ulemavu wa ngozi wanapata changamoto shuleni. Naomba nimhakikishie Mheshimwia Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali yetu hii ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan tumejipanga vyema katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kuishughulikia changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Wizara iko mbioni kutekeleza au kukamilisha mwongozo ambao utakwenda kushughulikia eneo hili la wanafunzi wetu wenye changamoto ya uoni hafifu, tukishirikiana na wenzetu wa Shirika Binafsi la Under the Same Sun. Kwa hiyo nimwondoe kabisa wasiwasi, kwamba mwongozo huo uko mbioni kuja na mara utakapokamilika na kusainiwa tutausambaza kwenye maeneo hayo ili kuhakikisha kwamba tunaitatua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie vile vile Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu tayari imeweza kusambaza vitabu vyenye maandishi makubwa kwa ajili ya wenzetu hawa ambao wana uoni hafifu. Kwa hiyo kule kwenye shule zetu zote za msingi pamoja na sekondari mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anazungumzia suala la miundombinu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mgawanyo wa fedha za UVIKO-19, zile ambazo tulizipata kupitia Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI zaidi ya Shilingi bilioni 2.4 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo zaidi ya 2200 kwa ajili ya wanafunzi wetu wenye mahitaji maalum kupitia hizi za UVIKO-19 na zile za GPE lenses na mchakato huu unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kupitia mradi wetu wa EP4R umeweza kujenga jumla ya matundu 4,549 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule zetu za msingi na sekondari. Tunaendelea kuboresha miundombinu hii kwa kuhakikisha na wao tunawatengenezea mazingira wezeshi ili isiwe changamoto kwao katika kupata elimu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.