Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kasalali Emmanuel Mageni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: - Je, ni lini barabara ya kutoka Magu – Bukwimba hadi Ngudu itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na Makao Makuu ya Mkoa wa Mwanza?

Supplementary Question 1

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa swali la aina hii limeshaulizwa na Mheshimiwa Shanifu Mansour, Mbunge wa Kwimba na swali la aina hii liliulizwa na Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Magu. Pia mimi mwenyewe niliwahi kuuliza swali la nyongeza kwenye swali la aina hii. Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri aliyetoa majibu leo, ilitoa majibu tofauti na iliyoyatoa leo kwa sababu, ilisema imeshatenga pesa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kilometa 10 katika mwaka huu wa bajeti na katika bajeti hiyo ilionekana. Sasa nataka kuuliza swali na kufahamu, je, Serikali katika ujenzi wa barabara hii inafahamu ni nini inahitaji kuwajibu watu wa Kwimba na Sumve au tunajibu tu ili muda uishe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; barabara hii imeshafanyiwa usanifu, kama majibu ya Serikali yalivyotolewa na kwa mujibu wa usanifu barabara hii, barabara mpya iliyosanifiwa itapita sehemu tofauti na inapopita barabara ya sasa katika eneo la Nkalalo ambapo kuna ujenzi wa reli ya SGR. Kwa sababu kwa mujibu wa ujenzi wa reli hii, hakuna barabara inaruhusiwa inaruhusiwa kupita juu ya reli. Ina maana reli hii ikimalizika kujengwa njia ya kutokea Kwimba kwenda Magu itakuwa imefungwa. Je, Serikali haioni kuna udharura wa kuanza ujenzi wa barabara hii ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo kutokea Kwimba kwenda Magu na kuiunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na Mkoa wa Mwanza kwa barabara ya lami? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Mageni Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika bajeti tuliyopitisha na bado sijaiondoa, tulitenga bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Katika jibu la msingi nimesema Serikali inaendelea kutafuta fedha na fedha ndio hii kwamba, tutakapopata sasa tutakuwa tunaanza ujenzi kwa sababu, hatujaanza, lakini ipo kwenye mpango na bado mpango huo haujafutwa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hakuna majibu tofauti, majibu ni hayo na ndio bajeti tuliyopitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, huu udharura anaousema Mheshimiwa Mbunge, naomba nimhakikishie kwamba, kama Wizara tunalichukua na wataalam watakwenda kufanya tathmini na kuangalia kama kinachosemwa kina ukweli, basi tutachukua ushauri na kulifanyia kazi kama kutakuwa na udharura huo. Ahsante.