Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Primary Question

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuvuna mamba katika Mto Ruvu hasa katika Vijiji vya Kigamila, Bwila juu, Magogoni, Bwila chini, Kongwa, Tulo, Lukuhinge, Kata za Mvuha na Serembala katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mamba hao?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na idadi kubwa ya vifo ya karibu watu 60 ndani ya mwaka mmoja na watu 30 kupata vilema vya kudumu, Serikali inakuja na majibu ya kusema kwamba inafanya tathmini. Ni tathmini gani ambayo inataka kuifanya ili kujiridhisha ili waende wakavune na ni lini watakamilisha hiyo tathmini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni lini Serikali itatoa kifuta machozi kwa watu ambao ndugu zao wamefiwa au wameliwa na mamba na wengine wamepata majeruhi? (Makofi)

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ufafanuzi katika eneo la kufanya tathmini. Maeneo ambayo anayaongelea Mheshimiwa Mbunge ni maeneo ambayo kiuhalisia, ni maeneo ya Mito na maeneo mengi ya Mito mamba wengi wanapenda kuishi maeneo hayo. Sekta ya Maliasili na Utalii tunahifadhi maeneo mbalimbali ambayo yanakuwa yamehifadhiwa. Lakini maeneo ya Mito ni maeneo ya mtiririko ambapo ukiangalia Mto kutoka eneo moja kwenda lingine ni eneo refu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunafanya tathmini kuangalia namna ya hawa mamba wanavyoishi majini kwa sababu, wanasafiri wanatoka njia moja kwenda njia nyingine. Unaweza ukamuona mamba yuko Morogoro lakini baada ya muda fulani ukamkuta yuko Pwani au yuko Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunafanya tathmini kuangalia hii namba ya hawa mamba ni kubwa kiasi gani. Kwa sababu, nao wana umuhimu fulani ambao katika maeneo hayo wanapaswa kuwepo sio kuwaondoa kabisa, kwa sababu vile vile, hiyo tunatambua kwamba ni moja ya maliasili ambayo inapaswa kuhifadhiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, tukishakamilisha tathmini tutaangalia kama idadi ni kubwa basi tutawavuna. Swali la kwamba ni lini ni pale ambapo tutakamilisha tathmini ambayo sasa hivi mchakato wake tumeshaanza na kama ambavyo nimesema ni Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Katavi na Rukwa ambako ndio inasemekana kuna mamba ambao wanasumbua sana. Ikishakamilika tu ndani ya mwaka huu wa fedha tutawavuna ama kuwapunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine ameongelea kuhusu kifuta machozi nimtoe wasiwasi tu Mbunge kwamba, suala la kulipa kifuta machozi tumelianza toka mwaka wa fedha ulioisha na sasa hivi kuna maeneo yanaendelea kulipwa. Kwa hiyo, hata kwenye eneo lake kama wananchi hawajapata kifuta machozi basi ninawaelekeza Idara ya Wanyama Pori, wataenda katika eneo hili na wataenda kulipa wale wananchi ambao wameathirika na tatizo hili. Ahsante. (Makofi)