Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka Mradi wa Ujazilizi katika Mkoa wa Manyara na Jimbo la Mbulu Vijijini ili kuwafikia wananchi wengi ambao hawakupitiwa na Mradi wa REA I, II na III?

Supplementary Question 1

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi anayofanya na Waziri mwenyewe kwenye Wizara hii. Lakini tatizo lililoko sasa REA inapokwenda kwenye kupeleka umeme vijijini zinapelekwa nguzo 20 tu na kwa sababu ni vijijini, nyumba ziko mbalimbali inatokea nyumba 10 tu zinapata umeme vijijini. Je, REA mnaonaje kwa nini msiongeze nguzo ili nyumba nyingi zikapata nguzo kuliko kupata nguzo hizo 20? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Waziri amekuwa akitoa taarifa ya wateja wanaotumia unit chini ya 70 kuuziwa unit kwa shilingi 100. Lakini sasa wateja hawa wanauziwa unit kwa shilingi 300. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa taarifa humu ili wananchi hawa wakajua nini hasa, umeme unatakiwa kulipiwa kwa hawa wateja wanaofikisha unit chini ya 70? (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya ngongeza ya Mheshimiwa Flatei kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumshukuru kwa pongezi alizozitoa kwa Wizara na kweli tunaendelea kujitahidi kwa maelekezo ya Serikali kuhakikisha tunatimiza maelekezo tunayopewa. Lakini nimpongeze kwa kufuatilia maeneo kwenye Jimbo lake na mimi nilienda kuzindua umeme na mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na nimuhakikishie kwamba nguzo 20 ni kwa wateja wa awali. Naomba uniruhusu nichukue nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge wote kwamba, tunapoendelea na mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili karibia kila eneo tumetoa kwa kuanzia nguzo 20. Lakini ni wateja tunawaita wateja wa awali sio kwamba ndio tumemaliza zoezi, kadri muda unavyozidi kuendelea TANESCO wataendelea kupeleka umeme katika maeneo hayo. Lakini pia REA wenyewe wataendelea kuongeza wigo wa kazi wanayoifanya kuhakikisha kwamba sasa watu wengi zaidi wanapata umeme katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kuhusiana na gharama za umeme. Kabla sijajibu kwanza nipende kutoa shukurani zetu kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuamua kuwapenda watanzania na kuwafikishia huduma ya umeme kwa gharama nafuu. Kwanza nguzo haziuzwi, mita haziuzwi, nyaya haziuzwi na connection ya umeme ni shilingi 27,000/= tu na hayo ndio maelekezo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye eneo la umeme mwaka 2016 zilitengenezwa Kanuni kulingana na mazingira tuliyokuwa nayo, ambazo zilikuwa zinasema waunganishiwaji wote wa umeme na watumiaji wa umeme wa maeneo ya vijijini watauziwa unit 1 kwa shilingi 100 endapo matumizi hayazidi unit 75 kwa mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maeneo ya Mijini hayakuwa yanahusika na utaratibu huu. Lakini baada ya kufikisha miundombinu mingi zaidi kwenye maeneo hata ya mjini tangu Disemba mwaka jana, Serikali imeelekeza popote pale ulipo ili mradi unatumia unit zisizozidi 75 gharama ya unit 1 itakuwa ni shilingi 100/=. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unipe nafasi ya kuwaelekeza Mameneja wote wa TANESCO nchi nzima, kukamilisha utaratibu ambao Serikali imeelekeza kupitia Wizara ya Nishati. Kuhakikisha watu wote wanaotumia umeme chini ya unit 75 kwa mwezi, kupata gharama kwa shilingi 9,150 ambayo ni unit moja ni shilingi 100. Na zoezi hili lilianza tangu mwezi wa saba. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri swali lake ni kwamba, Serikali haioni namna ambavyo wale wanatakiwa kuendelea kuuziwa? Maana yake umeme umepanda bei kwa swali la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba umeme sasa hauuzwi unit shilingi 100 umepanda. Sasa unampa maelekezo nani wewe ndio tunakusikiliza hapa, kwa nini umepanda yaani ndio swali lake. Kwa nini wasiendelee kuuziwa vile vile ile bei iliyokuwepo? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa ufafanuzi. Umeme haujapanda bei, kwa siku za hivi karibuni kumekuwa kuna utaratibu mpya wa kukusanya kodi ya majengo kupitia kwenye LUKU. Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuwaelimisha kwamba hizo sio gharama za umeme bali ni conduit tu ya kupitisha hizi gharama za upande wa pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye eneo la umeme, kilichotokea ni kwamba, utaratibu wa kuwaweka watu kwenye gharama ndogo ulikuwa haujafanyika. Kwa hiyo, watu waliwekwa kwenye gharama kubwa kwa maana ya kwamba waliwekwa kwenye viwango sahihi kwa mujibu wa Kanuni zilizokuwepo mwaka 2016. Sasa kuanzia Disemba mwaka jana Kanuni zilirekebishwa na utekelezaji unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba, wale wote ambao walikuwa wamepelekwa kwenye tunazoziita Tariff 1, Tariff 2 na Tariff 3, lakini gharama zao hazizidi unit 75 kwa mwezi warudishwe kwenye tunayoita D1 ambayo ni domestic one ambayo unit ni shilingi 100.

NAIBU SPIKA: Sasa ngoja, sasa hapo umeshajibu. Wewe kaa. Maana yake ni kwamba bei inatakiwa kuwa ni ile ile sasa wewe wasiliana na watu wako wa TANESCO huko, wasiwauzie bei zaidi ya ile iliyokuwepo mwanzo ndio jibu lako hapo. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa kama utaendelea kupata changamoto huko Mbulu Vijijini bila shaka utampigia simu Mheshimiwa Naibu Waziri, ili awaeleze hao wa huko Mbulu Vijijini waliopandisha hiyo bei. (Makofi)