Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Nyashimo Wilayani Busega hadi Dutwa Wilayani Bariadi kupitia Shigala, Malili, Ngasamo na Imakanate yenye kilometa 47 kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nikupongeze wewe kwa kutaja jina langu vizuri na nimkumbushe tu Naibu Waziri, naitwa Simon Songe Lusengekile.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa barabara hii inachochea sana uchumi wa wananchi wa Jimbo la Busega na Jimbo la Bariadi, kwa maana ya Ngasamo, Shigara, Dutwa pamoja na Mariri.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu sana wa kuipa kipaombele barabara hii ili iweze kutengeneza kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tunaelekea sasa mwisho wa Bunge letu la Bajeti; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutembelea Jimbo la Busega ili aone umuhimu wa hii barabara? (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lusengekile, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana na ndiyo maana kwanza Mheshimiwa Mbunge tayari kuna fedha zipo anajengewa madaraja mawili hapa kama nilivyoyataja katika jimbo lake. Lakini, la pili tumeahidi kwenye jibu langu la msingi kwamba barabara hii inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka huu wa fedha ambao unaanza Julai ambayo ni keshokutwa. Kwa hiyo, hii ikikamilika tutajenga barabara hii kwa kiwango cha lami tunajua umuhimu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili mimi niko tayari kufanya ziara kule Busega. Kwanza kuna shemeji yangu pale kwa hiyo nitaenda kumsalimia. Tuko tayari, tutaambatana. Ahsante sana.