Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, ni lini Hospitali ya Wilaya ya Rorya itaanza kutoa huduma?

Supplementary Question 1

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na nishukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba nipate nafasi sasa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza ambayo kimsingi yanatokana na jibu la swali la msingi.

Swali langu la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba mwaka 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 500 kilichangwa kwa ajili ya kununua vifaa tiba, lakini sasa tumebakiza mwezi mmoja unaokuja wa sita.

Je, ni lini Serikali sasa hii milioni 500 iliyokuwa imetengwa itaweza kufika kwenye hospitali hii ili kuweza kununua vifaa tiba hivi ili kuongeza wigo wa utoaji huduma katika hospitali ile?

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, kwa kuwa Serikali imekiri mwezi Disemba mwaka huu hospitali ile itafunguliwa kwa ajili ya kutoa huduma lakini pia inakiri kwamba hatuna jengo la upasuaji na wala halijaanza kujengwa; je, jengo hili ni lini litaanza kujengwa ili itakapofika mwezi Desemba hospitali ile iweze kutoa huduma inavyotakiwa? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Kimsingi tumetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya hospitali zote 67 za Halmashauri za awamu ya kwanza ikiwepo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na fedha hizo tayari zimeshapelekwa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kwa ajili ya kununua vifaa tiba ambavyo Halmashauri ya Rorya wameainisha kwamba ni mahitaji yao ya kipaumbele.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hizo tayari zimekwishatolewa kwa ajili ya Hospitali ya Rorya ana tayari zimekwishawasilishwa MSD, taratibu za manunuzi ya vifaa tiba zinakamilishwa na vifaa tiba vitaletwa katika Halmashauri ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na jengo la upasuaji; hospitali ile tayari ina majengo saba, tunaendelea na ujenzi wa majengo tisa na kati ya majengo saba ambayo tayari yamekamilika kwa asilimia 98, jengo la akina mama wajawazito linaungana na jengo la upasuaji. Kwa hiyo, tayari tuna jengo la upasuaji la kuanzia katika Hospitali ya Wilaya ya Rorya. Mpango ni kuendelea kujenga majengo mengine ya upasuaji katika mwaka wa fedha ujao, lakini hili halitaathiri kuanza kutoa huduma za upasuaji ifikapo Disemba mwaka huu 2021, ahsante sana.