Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Primary Question

MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Igunga – Miswaki – Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida yenye urefu wa kilometa 89?

Supplementary Question 1

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante; pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, barabara hii ambayo inatoka Wilaya ya Igunga kuja Loya mpaka Magulyati ni barabara muhimu kwenye uchumi wa wananchi wa Jimbo la Igalula, lakini barabara hii ina mito zaidi ya tisa, kwa tafiti ya mkandarasi inasema kila mto mmoja kwa kujenga box culvert inagharimu takribani shilingi milioni 100. Leo Waziri ananiambia ametenga milioni 200 maana ma-box culvert mawili tu hela itakuwa imekwisha.

Je, Serikali haioni haja ya kuitilia kipaumbele kuiongezea fedha hii barabara ili wananchi waweze kupita masaa yote? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, barabara hii ina vigezo na imekidhi vigezo vya kupandishwa hadhi ihudumiwe na TANROADS kwa sababu inaunganisha Wilaya mbili ya Igunga na Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, lakini vilevile inaunganisha na Mkoa wa Tabora na Singida. Kwa nini Serikali isipitie mchakato kuipandisha hadhi iweze kuhudumiwa na TANROADS ili kuepuka bajeti ndogo ya TARURA? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Venant Daudi Protas, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Igalula na barabara hii imepitiwa na mito mingi na kama ambavyo nimeongea kwenye jibu langu la msingi, Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 600 katika mwaka wa fedha 2021 tunaomaliza lakini katika mwaka wa fedha unaokuja. Jumla ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kutambua umuhimu wa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie pamoja na ma-culvert ambayo tumeendelea kujenga lakini tathmini itafanyika katika maeneo mengine yote ya barabara ile ambayo yanahitaji kujengewa ma-culvert lakini pia na madaraja ili fedha iweze kutafutwa na iweze kutengwa kwa ajili ya kujenga madaraja hayo kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, barabara zote ambazo zinahitaji kupandishwa hadhi kwenda kuwa barabara za TANROADS utaratibu upo wazi unaanza katika ngazi ya Halmashauri husika DCC tunakwenda RCC na baadae unawasilishwa katika Wizara za TAMISEMI na Ujenzi.

Kwa hiyo, naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba wafuate utaratibu huo ili tuweze kuona kama inakidhi vigezo iweze kupata hadhi inayotakiwa, nashukuru sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini nilitaka kuongeza kwenye majibu yake kwa mara ya kwanza Serikali imesikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge kwa sababu fedha za TARURA zilikuwa zinatoka katika Mfuko wa Barabara, kwa mara ya kwanza tumepata fedha shilingi bilioni 172 kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu fedha hizi tumezipata haraka haraka na bajeti zilishapitishwa na Kamati za Halmashauri, kwa hiyo tumetumia maamuzi ya jumla kila Jimbo tunapeleka shilingi milioni 500 TARURA kwa ajili ya ujenzi wa barabara. (Makofi)

Kwa hiyo, Halmashauri au Waheshimiwa Wabunge mtaamua milioni 500 kujenga kilometa moja ya barabara ya lami au milioni hiyo 500 kujenga kilometa 10 kupandisha barabara ya udongo kuwa ya changarawe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeiweka hii chini ya uamuzi wa Mabaraza ya Madiwani kuamua milioni hii 500 kwa kila Jimbo sio kwa kila Halmashauri. Kwa hiyo, kama Halmashauri ina Majimbo matatu kila Halmashauri itapata milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Na hii ndiyo kazi ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesikia kilio chenu Waheshimiwa Wabunge na Waziri wa Fedha ananiambia bado wanaangaliaangalia kwa hiyo mambo yanaweza yakawa mazuri zaidi. (Makofi)