Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa Hati katika Mradi wa Urasimishaji kwa Wananchi wa Kata za Kibamba, Kwembe, Mbezi, Msigani, Goba na Saranga?

Supplementary Question 1

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali yanayoridhisha kwa wastani, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, majibu ya Serikali yanaeleza wazi juu ya utoaji wa hati 845 tu kati ya upimaji uliokamilika wa watu 100,041 asilimia 0.0056 katika kipindi chote cha miaka miwili. Je, Serikali haioni sasa ni muda sahihi wa kupunguza lile tatizo la premium ambalo linasababisha bei kubwa kwa wananchi ambao wanashindwa zaidi ya ile 180,000 ambayo wamelipa kwa wale wa kampuni? Sasa hapa ni kupunguza ile premium.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni kweli kwenye majibu ya msingi inasema wachangiaji ni 30,000, lakini kwa taarifa nilizonazo kama Mbunge ni zaidi ya wachangiaji 80,000. Kwa hiyo, jumla ya fedha ni bilioni nne wanazisema, mimi nasema bilioni 15. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kupeleka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ili akafanye ukaguzi maalum tuje na takwimu zilizo sahihi kwa ajili ya fedha za wananchi zilizopotea? (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimsahihishe, si kweli kwamba, hati 847 tu ndio zimeandaliwa. Kwenye jibu langu la msingi nimesema hati 1,754 kati ya waombaji 1,925 tayari zimeandaliwa na wamechukua, lakini tunaendelea kuandaa hati kwa sababu, viwanja vilivyokamilika ni 8,316 kwa hiyo sio 845 kama alivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumzia suala la kupunguza premium kwamba, pengine wananchi wanashindwa kuchangia. Naomba tukumbuke tu kwamba, premium hii awali ilikuwa ni 15% kwa viwanja vyote. Ikapungua ikawa 7.5%, lakini badaye Wizara ikapunguza zaidi kwenye zoezi la urasimishaji wanalipa 1% ya premium ambayo wanatakiwa kulipa tofauti na ule upangaji wa kawaida, ilitoka 7.5% wao wanalipa 2.5%. Kwa hiyo, kama ni suala la kupunguza ni kweli upunguzaji tumepunguza, lakini kwa sababu ni hoja inatolewa na Serikali ni sikivu basi tutaona namna kama kuna haja ya kupunguza tena au tuendelee na ileile 1%. Tukumbuke kodi hizi pia ndio zinarudi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili amezungumzia kwamba, pesa ambazo zimekusanywa tulizotoa takwimu hapa ni tofauti. Si kweli anachosema, kwa mitaa mitano haiwezi kukusanya bilioni 15 kwa zoezi la urasimishaji, ukizingatia kwanza walipaji wenyewe ni wachache na nimetaja kati ya waombaji 147,000 tunaoshughulika nao sasa hivi ni 1,925 tu ambao wamekamilisha malipo yote. Kwa hiyo, si kweli kwamba, kuna pesa nyingi ambazo zipo,

Mheshimiwa Naibu Spika, kama pengine Mheshimiwa Mbunge anajua kuna mahali ambapo kuna pesa zimekusanywa na pengine hazijulikani zilipo, ameomba ukaguzi ufanyike, tutalifanyia kazi ili tuweze kujua ukweli wa Mheshimiwa Mbunge aliouleta na takwimu tulizonazo Wizarani ili tuweze kuwa na uhakika na alichokisema. Ahsante.