Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Primary Question

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:- Je, ni kwa nini Mgodi wa Mwadui Williamson Diamond Limited umesimamisha shughuli za uzalishaji wa almasi kwa muda mrefu na ni lini mgodi huo utaanza uzalishaji tena?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana kwa majibu ya Serikali yaliyotolewa na Naibu Waziri. Kwanza nipongeze kwa jitihada hizi ambazo zinaendelea, lakini bado lipo tatizo kubwa la hizi benki ambazo Mgodi wa Mwadui umekwenda kwa ajili ya kuomba mkopo huu ilimradi uanze uzalishaji kwa mara nyingine. Jambo kubwa linalohitajika hapa ni hii corporate guarantee ambayo inatakiwa itolewe na Petra ambaye ndiye kimsingi mwekezaji wa Mgodi huo wa Mwadui, lakini jambo ambalo nadhani ni zuri zaidi kwa Serikali ni kuhakikisha inazungumza ama inakaa kwa karibu na Petra, ilimradi suala hili la corporate guarantee liweze kutolewa na Petra na badaye utaratibu wa kutolewa fedha na ili mgodi uweze kuzalisha ufanyike haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, liko tatizo kubwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Serikali yenyewe, lakini pia na suala zima la Service Levy pamoja na CSR ambayo imekuwa ni msaada mkubwa kwa shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Kishapu. Ni lini sasa Serikali itakwenda kusimamia na kushirikiana na hawa ma-banker ilimradi benki hizi ziweze kutoa fedha na kuweza kuzalisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa swali la pili nenda moja kwa moja kwenye swali.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, wako watumishi zaidi ya 1,200 pale katika Mgodi wa Mwadui na changamoto kubwa ya hawa watumishi ni mishahara yao kusimama kwa muda mrefu. Sasa ipo sababu ya Serikali kuona umuhimu wa mgodi huu kuhakikisha unaanza uzalishaji, ili adha na matatizo makubwa ya watumishi hawa waliopo katika Mgodi wa Mwadui waondokane na adha hii kubwa. Ahsante sana.

Name

Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mbunge pia kwa kutambua kwamba, Wizara inafanya kila linalowezekana kuona kwamba, mgodi huu unarejea katika hali ya uzalishaji. Kwa swali lake la kwanza, lakini pia ni kweli kwamba, natambua Wizara itafanya kila linalowezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza uzalishaji wa almasi Tanzania tunaongea habari ya Mgodi wa WDL ndio kiini kikubwa cha uzalishaji wetu wa almasi. Pia, tunatambua adha ambayo watumishi wanapata kwa kushindwa kulipwa mishahara, lakini pia tunatambua kwamba, kama uzalishaji hautafanyika kwa muda mrefu maana yake ni kwamba, hata shimo lile tunapochimba litaanza ku-cave in na kwa hiyo, gharama ya kuja kuanzisha mgodi mara nyingine itakuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Madini itafanya kila linalowezekana, iwe ni kuongea na watoa huduma, iwe ni kuendelea kufanya ushawishi wake kwa ajili ya benki za hapa nchini na hata kuongea na Petra, ili ikiwezekana basi turejee katika uzalishaji. Mara tutakapoanza uzalishaji maana yake ni kwamba, matatizo yote aliyoyaainisha Mbunge ya adha ya watumishi kutolipwa pamoja na service levy vyote vitakuwa vinapatiwa suluhisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara itafanya kila njia inayowezekana; yaweza kuwa ni ushawishi kwa benki zetu, hilo moja, au kukaa na watoa huduma ili kwamba, wakubali kufanya hata kwa kukopwa ili baadaye tuzalishe halafu tuuze. Njia zozote ambazo zinaweza zikarejesha uzalishaji katika Mgodi wa WDL tutazi-pursue ili kwamba, tuweze kurejesha hali ya uzalishaji katika Mgodi wetu wa Almasi Tanzania. Ahsante.