Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Primary Question

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:- Je, ni lini watumishi waliohamishiwa Halmashauri ya Uvinza kutoka Halmashauri ya Kigoma Vijijini watalipwa stahiki zao?

Supplementary Question 1

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa NaibU Spika, Waziri haoni kwamba kwa namna moja au nyingine anasababisha watumishi hawa kufanya kazi katika mazingira magumu na hasa muda ni mrefu maana Halmashauri ile imeanzishwa mwaka 2013 na tayari kuna baadhi ya watumishi wamekwishastaafu. Kwa hiyo naomba commitment ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo hili hawa wananchi wapiga kura wangu wanakwenda kulipwa lini fedha hii? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kusema katika majibu yangu ya msingi kwamba tunatambua madeni ya watumishi wetu katika Halmashauri ya Uvinza na Serikali imeendelea kuweka mipango kwa maana ya kutenga fedha kwenye bajeti ili kuhakikisha kwamba hayo madeni yatakwenda kulipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni haya yanalipwa kwa kutumia fedha za matumizi mengineyo kwa maana ya OC, lakini pia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.

Na hivyo tunaendelea kuwaelekeza Wakurugenzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwa muktadha huu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza waanze kutenga fedha kwa ajili ya kuwalipa watumishi wale madeni yao kwa awamu ili watumishi wale sasa waweze kufanya kazi kwa kuwa na motisha kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba na Serikali pia inaendelea kufanya uhakiki wa madeni hayo na kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunawalipa wale watumishi stahiki zao za yale madeni.