Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ahmed Yahya Abdulwakil

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Primary Question

MHE. AHMED YAHYA ABULWAKIL aliuza:- Je, ni lini Serikali itawaunga mkono wananchi wa Chukwani waliojitolea kujenga Kituo cha Polisi cha ghorofa moja kwa kumalizia ujenzi wa kituo hicho?

Supplementary Question 1

MHE. AHMED YAHYA ABULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na yenye tija, naipongeza Serikali kwamba hivi karibuni itapata kituo kile na kuondokana na gharika ya majambazi waliovamia miaka ya nyuma. Kwa sababu hiyo, nashawishika kumwuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Kwahani Eneo la Ng’ambo Jimbo la Kwahani ni Kituo cha Polisi cha muda mrefu tangu ukoloni; na kwa sasa hakikidhi mahitaji kuhudumia wananchi wakati huu: Je, Serikali ina mpango gani wa kukitanua ili maofisa wetu waweze kufanya kazi kwa utulivu na ufasaha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba, hivi karibuni Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amezindua soko jipya la kisasa eneo la Kibanda Maiti au tunaweza kusema Kibanda cha Demokrasia; linahudumia zaidi ya watu 10,000 usiku na mchana: Je, Wizara yako ina mpango gani kulinda usalama wa raia na mali zao? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa na wananchi wake hawakukosea kumchagua. Ninafahamu Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele kwenye kuchangia maendeleo iwe kwenye elimu au vituo hivi vya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali lake, ninafahamu pia kwamba hii miji inapanuka na ongezeko la watu linakuwa kubwa. Ongezeko hili linaendana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ulinzi. Kwa hiyo, niendelee tu kumsihi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla tuendelee kuhamasisha wananchi kwamba jukumu la ulinzi ni letu wote ili tuweze kushirikiana kwanza kuhakikisha kwamba tunafanya maboresho makubwa katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa ya Serikali imefanyika; yako maeneo mbalimbali ambayo ujenzi umeendelea kukamilishwa na kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kwamba Mfuko huu wa Tuzo na Tozo umefanya kazi kubwa. Katika mwaka 2020/2021 peke yake zaidi ya nyumba 431 zimekamilishwa ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira mazuri ya askari wetu kufanya kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuhamasisha wananchi na Serikali kupitia mfuko huu tutaendelea kufanya maboresho makubwa.

Mheshimiwa Spika, mkakati tunaoufanya katika eneo hili la Kibanda Mauti, ni kweli kwamba kuna doria zinafanyika, wale wanaojihusisha na uhalifu wanaendelea kukamatwa na kufikishwa kwenye taratibu zetu za kisheria, lakini pia tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, tunaendelea kuwashirikisha wananchi ili waweze kusaidia katika ulinzi na tunaendelea pia kushirikiana na vyombo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe maelekezo kwa Jeshi la Polisi kule Zanzibar, washirikiane na Uongozi wa Soko katika eneo Mheshimiwa Mbunge amelitaja ili tupate eneo ambalo sasa tutaanza mkakati wa kujenga kituo katika eneo hili kwa sababu changamoto zimeongezeka na idadi kubwa ya watu katika maeneo haya na kuwepo kwa soko kunahitaji ulinzi madhubuti. Ahsante sana. (Makofi)