Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:- Je, lini ni Serikali itatekeleza ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni ya kumaliza mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wananchi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege KIA?

Supplementary Question 1

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Hai. Mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu sana, jambo linalosababisha wananchi kukosa maeneo ya malisho na kuishi kwa wasiwasi kwenye maeneo yao ambayo wanaishi pale tangu mwaka 1975. Wananchi wote wa vijiji hivi vyote vinne vinavyotajwa, wana usajili wa vijiji vyao, nikimaanisha Kijiji cha Sanya station, Tindigani, Mtakuja na Chemka.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ukizingatia eneo lililopo kwenye uwanja huo ni kubwa sana; kwenye list ya Viwanja vya Ndege tulivyonavyo hapa Tanzania, Kiwanja cha Kilimanjaro Airport kinaongoza kikifuatiwa na Kiwanja cha Dodoma na Songwe, halafu kiwanja cha nne ni Dar es Salaam.

Je, Serikali haioni kwa ukubwa ulioko pale, iko haja ya baadhi ya maeneo yarudi kwa wananchi ili waweze kuendelea na maeneo yanayobaki, yabaki kwenye Uwanja huu wa Ndege jambo ambalo tayari mimi mwenyewe nilishakutana na Management na wakaonyesha utayari wa kukubaliana na jambo hili?

Swali la pili: Je, Kwa kuwa mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu, Serikali haioni iko haja sasa wa kufikia mwisho na Mheshimiwa Naibu Waziri sasa tuambatane tukakae na wananchi wale tumalize mgogoro huu ili kesi hii iishe na wananchi waendelee na maisha yao; na kwa kuzingatia kwamba wananchi hawa ni wema sana, walitupa kura nyingi za Chama cha Mapinduzi na pia Diwani aliyeko pale alipita bila kupingwa? Ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu na hapo nyuma kulikuwa kuna changamoto kwamba vijiji vilipima maeneo yao yakaingia katikati ya uwanja ambao tayari ulikuwa una hati. Changamoto hiyo tayari tulishairekebisha na zile ramani za vijiji vile zilifutwa ili ramani ya uwanja wa ndege ibaki na ndivyo ilivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa ni kweli kwamba uwanja ule ni mkubwa lakini uwanja ule ulitolewa vile na muasisi wa Taifa baba yetu Julius Kambarage Nyerere na kile kiwanja kina mipango mahsusi ya kuweka viwanda vya kitalii na viwanda vinavyohusiana na viwanja vya ndege. Biashara zote za viwanda vya ndege, sasa hivi pale kuna mpango wa kuanzisha aviation school ambapo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kimekwishajidhatiti na vile vile tuna mpango na hawa watu wa TAA ili kuweka majengo ya kuhifadhi mipango ambayo imepangwa pale. Kwa hiyo ningependa kumshauri Mheshimiwa Mbunge pamoja na wale wananchi wa Hai wajipange kuanzisha biashara zinazohusiana na viwanja vya ndege kuliko kupanga kuugawa uwanja wa ndege ule kwenda katika vijiji.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kwamba Wizara yangu iko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda pale kuongea na kumaliza suala hilo kwani tumejipanga mwaka huu tuweze kufika pale kufanya tathmini na kumaliza suala hilo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.