Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalinda Akinamama wanaochenjua dhahabu dhidi ya sumu ya zebaki ambayo ina madhara makubwa kiafya?

Supplementary Question 1

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mbali tu na tatizo la kemikali ya zebaki, lakini wachimbaji wadogo wamekuwa na tatizo kubwa sana la mitaji wakiwemo wachimbaji la Nyamongo Mkoa wa Mara. Ni lini sasa Serikali watawawezesha wachimbaji wadogo wa Nyamongo hasa vijana na akinamama ili waweze kuchimba vizuri dhahabu zao.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kuhusiana na kemikali zinazodhuru wananchi, si tu kwa wachimbaji wadogo mbali na kwa wananchi wanaozunguka migodi. Sasa wananchi wa Nyamongo wameathirika sana na mara nyingi Serikali imesema italipa fidia, ni lini sasa itawafidia wananchi ambao wameathirika na kemikali zinazotoka migodini?

Name

Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu mitaji Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanya lile linalowezekana kuhusisha benki zetu za ndani ambazo zimehiari kutoa mitaji kwa ajili ya wachimbaji wetu wadogo na kwa taarifa mwezi wa Sita Mheshimiwa Waziri wa Madini alizindua NMB Mining Club ambapo wateja wachimbaji wadogo wanaweza wakaenda pale na wakakopeshwa.

Mheshimiwa Spika, pia benki zetu zingine za ndani zimehiari tayari na tayari tumeona kwamba wanashiriki katika shughuli za kuwakopesha wachimbaji wadogo. Ambacho tumewaasa wachimbaji wadogo ni kwamba kabla ya kwenda benki awe na leseni halali, inayotambulika na Tume ya Madini, lakini pia awe basi na takwimu za kazi anazozifanya ionekane kwamba unaonekana ukizalisha, ukiuza unapata faida benki wamehiari kutoa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo limefanyiwa kazi kwa namna hiyo na wachimbaji wadogo wameanza kupata matunda. Pia kwa taarifa benki zetu za ndani zimekwenda mbali zaidi hadi kutoa fedha kwa ajili ya miradi mikubwa. Kwa hiyo tunadhani kwamba, hiyo ni hatua na suala la mitaji limeendelea kushughulikiwa halimradi wachimbaji wetu wadogo waweze kutoa ushirikiano kwa jinsi hiyo.

Mheshimiwa Spika, suala la mazingira yanayozunguka migodi. Ni kweli kwamba inapokuja kwenye mgodi ambao Mheshimiwa Mbunge ameutaja, Serikali imeendelea kufanya hatua, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna tena maji yanayotiririshwa katika maeneo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, limeendelea kushughulikiwa na timu yetu ya Wizara ya Madini pamoja na NEMC pamoja na watu wa Wizara ya Maji, wamekuwa wakishirikiana katika kufanya ukaguzi kuhakikisha kwamba hakuna uchafu tena unaoendelea kutiririshwa kutoka katika migodi.

Mheshimiwa Spika, suala la fidia pia limeendelea kufanyiwa kazi na yule Mthaminishaji Mkuu wa Serikali. Ahsante.