Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatafuta mkakati wa kudumu wa kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mkoa wa Lindi?

Supplementary Question 1

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali pia napongeza kazi inayofanywa na Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi na Halmashauri zake katika kutatua migogoro hii.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni lini itajenga mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo hiyo? Hapa tumeona katika jibu la msingi shida kubwa ni kugombania maji pamoja na malisho.

Mheshimiwa Spika, pili, tunaomba kazi hii ya kutatua migogoro katika Mkoa wa Lindi iharakishwe maana Sekretarieti ya Mkoa imeelemewa na migogoro hiyo. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tecla, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kutambua umuhimu na katika mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, katika bajeti ya mwaka huu 2021/2022 tumetenga jumla ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya kujenga mabwawa katika Mkoa wa Lindi. Bwawa moja litajengwa katika Wilaya ya Liwale na lingine katika Wilaya ya Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Lindi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga vyema kwa kutumia Kamati inayoshughulikia migogoro ya ufugaji na wakulima kwenda kuweka kambi kuzungumza nao na kushirikiana katika kutafuta mbinu za kusuluhisha migogoro hii, ikiwa ni pamoja na kutatua lile tatizo la nyanda za malisho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.