Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI Aliuliza: - Serikali ilichukua eneo la Mlima Nkongore ambao ndani yake kulikuwa na makazi ya wananchi na kuliwekea beacon na kusababisha kaya zaidi ya 10 zilizochukuliwa maeneo hayo kuishi kwa hofu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzilipa fidia Kaya hizo?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza; kwa kuwa eneo lote lile la mlima lilikuwa la kijiji na kwa kuwa sheria zetu za ardhi haziruhusu mtu kwenda kuvamia kijiji au Kamati ya Ulinzi kwenda kutwaa eneo la kijiji na kuligawia taasisi nyingine, ile ni mali ya wanakijiji.

Sasa ni lini taasisi hiyo iliyotwaa eneo la wanakijiji watalipa fidia ya kaya 10 ambazo zilikuwa zinafanya kazi pale? Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa migogoro ya ardhi Mkoa wa Mara imekuwa mingi sana na hata juzi tumesikia Rorya pale kuna mtu amekufa kwa migogoro ya ardhi. Ni lini sasa Serikali itaenda kupima hasa vijiji 30 vya Tarafa ya Chamriho, Jimbo la Bunda kuwapa Hati ya Kimila?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Getere kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza Sheria ya National Environmental Management Act No. 20 ya 2004 hairuhusu maeneo yale ambayo ni hatarishi kama milima na maeneo ya kingo za mito kuweza kumilikiwa na wananchi, yanakuwa ni protected chini ya usimamizi wa Waziri wa Ardhi. Kwa hiyo, eneo la mlima analolizungumzia si halali kwa watu kumilikishwa pale na litabaki under protection kama ambavyo Kamati ya Usalama ya Wilaya imekwishaelekeza kuwapa watu wa Magereza kuliangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na vijiji 30 kuhusu suala zima la kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi; kama nilivyojibu juzi, ni suala tu la mamlaka yenyewe ya upangaji, pale watakapokuwa tayari sisi kama Wizara kupitia Tume ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi tutakuwa tayari kushirikiana nao kwa sababu kadri wanavyopima na kuweka mpango wa matumizi katika vijiji vyao, ndivyo jinsi ambavyo wanapunguza migogoro ya ardhi kwa watumiaji ardhi katika maeneo. Kwa hiyo, sisi tupo tayari wakati wowote pale ambapo Halmashauri itakuwa tayari kufanya kazi hiyo, waangalie kama bajeti wanayo, tutakwenda kuwasaidia, ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilipata fursa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita nilienda kutembelea eneo hilo na bahati nzuri tulikuwa na Mbunge husika na zile kaya tuliweza kuzibaini pale katika eneo lile. Tulichokifanya na Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya tukasema kwamba wale ambao kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira maana yake hakuna compensation isipokuwa nini utaratibu wa busara ufanyike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hilo tumeliacha chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, DC wetu wa Tarime linafanyiwa kazi lakini utaratibu wa kulitangaza eneo lile kuwa eneo lindwa, utaratibu huo kwa mujibu wa Kanuni zetu tunaenda kubadilisha Kanuni hivi sasa si muda mrefu tutatangaza baadhi ya maeneo likiwemo eneo la Mlima Nkongore, ahsante sana.