Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ali Salim Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mwanakwerekwe

Primary Question

MHE. ALI SALIM KHAMIS aliuliza:- (a) Je, Shirika la Ndege Tanzania ni Shirika la pamoja kati ya Tanganyika na Zanzibar? (b) Kama ndiyo je, Zanzibar ina asilimia ngapi katika Shirika la ATCL? (c) Je, ni lini ATCL italipa deni la kodi ya kutua (landing fee) kwa Mamlaka ya Ndege Zanzibar?

Supplementary Question 1

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa katika umiliki wa Benki Kuu ya Tanzania, Zanzibar imeainishwa wazi kwamba inamiliki asilimia 12, ni vipi leo Waziri anatuambia Shirika hili la Jamhuri ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara au Tanganyika, haikuainishwa asilimia za umiliki wa Shirika hili. Je, siyo njia ile ile ya kuendelea kuinyonya Zanzibar na kuinyang‟anya haki zake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili…
SPIKA: Mheshimiwa kabla maswali yako hayajaendelea, una chanzo cha hizo asilimia zinazonyonywa, una reference yoyote au ni mawazo yako wewe?
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Spika, amesema Naibu Waziri hapa kwamba Shirika linamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa asilimia 100, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, lazima tujue asilimia zinazomilikiwa na Serikali ya Zanzibar, tujue Wazanzibari haki zetu zi zipi, kama ilivyoainishwa katika Benki Kuu kwamba Zanzibar inamiliki Benki Kuu kwa asilimia 12.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo swali langu namwomba Waziri asikwepe hili suala, atuainishie hisa za Zanzibar ni kiasi gani katika ATCL kwa sababu hapo mwanzo Shirika hili lilikuwa ni ATC na wamiliki walikuwa ni hao hao Serikali, kwa hiyo imetoka Serikali halafu ikajibinafsishia Serikali… (Makofi)
SPIKA: Swali la pili!
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Spika, swali la pili, Naibu Waziri amesema kwamba deni la kutua kwa ndege ya ATCL, kwa muktadha ule ule wa kuinyang‟anya Zanzibar haki zake, ndege hii inatua katika viwanja vya ndege vya Zanzibar na hailipi kodi na hapa Mheshimiwa Naibu Waziri ametaja deni ambalo lipo, lakini bado anatuambia kwamba mpaka CAG alihakiki wakati wanajua kwamba walikuwa wanatua Zanzibar na hawalipi kodi…
SPIKA: Swali ni nini?
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Ni lini deni hili litalipwa kwa Serikali ya Zanzibar haraka iwezekanavyo, kwa sababu deni hili ni la siku nyingi? Ahsante

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, siyo Serikali ya Tanganyika. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina uwezo wa kumiliki na ndiyo maana inamiliki hisa asilimia 100 za ATCL ambayo tuliibinafsisha huko nyuma na sasa tumeirudisha na tunataka kuirekebisha zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu deni, tumelitaja, haya madeni ni ya siku nyingi, ni ya Shirika ambalo lilishakufa, ATC, sasa tuko kwenye kampuni ATCL, lakini tunasema deni hili likishahakikiwa, litalipwa na ndege za ATCL zitakapoendelea kutua landing fee ya kila kiwanja italipwa.

Name

Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. ALI SALIM KHAMIS aliuliza:- (a) Je, Shirika la Ndege Tanzania ni Shirika la pamoja kati ya Tanganyika na Zanzibar? (b) Kama ndiyo je, Zanzibar ina asilimia ngapi katika Shirika la ATCL? (c) Je, ni lini ATCL italipa deni la kodi ya kutua (landing fee) kwa Mamlaka ya Ndege Zanzibar?

Supplementary Question 2

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Tanzania tunayo makampuni binafsi mawili yanayotoa huduma za ndege kwa wasafiri hapa nchini, FastJet pamoja na Precision.
Mheshimiwa Spika, lakini ningependa kujua ni utaratibu gani wa gharama za nauli wanazotumia kupanga. Kwa sababu gharama ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kurudi inakaribia shilingi 800,000 vivyo hivyo gharama ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya inakaribia shilingi 800,000 sawasawa na nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dubai kwa ndege za Emirates. Nataka kujua, ni utaratibu gani unaotumika kupanga gharama za nauli kwa wasafiri hasa kwa Dar es Salaam, Mwanza pamoja na Mbeya, routes za ndani hizi ni nani anayepanga nauli hizi?

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nauli za ndege kwa sasa zinapangwa na soko.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kinachotokea taasisi yetu ya SUMATRA huwa inafanya kazi ya kuangalia kama hizo nauli ambazo hupangwa na soko na pengine soko haliko sawasawa inafanya utaratibu wa kurekebisha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho Serikali imeamua ni kufufua Shirika letu la ATCL liwe na ndege za kutosha ili tuweze kuondoa ukiritimba wa kampuni chache zinazotoa huduma za ndege kwa sasa, hatimaye bei ya soko iwe kweli bei ya soko. (Makofi)


SPIKA: Majibu ya nyongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri zinapangwa na soko lakini Mamlaka ya TCA (Tanzania Civil Aviation) ndiyo inasimamia jambo hili. Kwa kulijua hili, Serikali inafanya kila linalowezekana tuweze kufufua Shirika la Air Tanzania na ambapo sasa tuna utaratibu wa kununua ndege mbili, Q400, wakati wowote zitaweza kufika hapa Tanzania kuhakikisha kwamba bei hiyo sasa tunaisimamia ipasavyo.

Name

Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Primary Question

MHE. ALI SALIM KHAMIS aliuliza:- (a) Je, Shirika la Ndege Tanzania ni Shirika la pamoja kati ya Tanganyika na Zanzibar? (b) Kama ndiyo je, Zanzibar ina asilimia ngapi katika Shirika la ATCL? (c) Je, ni lini ATCL italipa deni la kodi ya kutua (landing fee) kwa Mamlaka ya Ndege Zanzibar?

Supplementary Question 3

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina swali dogo tu, najua kuna juhudi nzuri sana za kufufua Shirika letu la Ndege hili la ATCL, lakini lipo tatizo kubwa la wafanyakazi wasiokuwa na tija. Ndege hizo mbili zinazotarajiwa kununuliwa kuna wafanyakazi zaidi ya 200, ni lini sasa au mna mkakati gani wa kupunguza wafanyakazi wasiokuwa na tija ili hizo ndege mbili zitakazonunuliwa ziwe na manufaa kwa Shirika la ATCL?

Name

Prof. Makame Mnyaa Mbarawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkoani

Answer

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli ATCL kuna wafanyakazi takribani 200 na sasa hivi kuna ndege moja, tunalolifanya sasa hivi ni kuhakikisha wafanyakazi wote tunawaajiri upya kuhakikisha tunakuwa na wafanyakazi ambao wanaendana na ndege zilizopo. Hatutaki kuchukua watu ambao wanakaa wanapiga maneno, lakini hakuna kazi ambayo inafanywa.