Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani kutatua migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi wa Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba?

Supplementary Question 1

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuongeza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nini tamko la Serikali kutokana na wawekezaji hawa wakati mwingine kujichukulia sheria mkononi na kuwafungulia watu kesi na kuwaweka ndani ikiwa hata wao hawafuati Sheria ya Ardhi, ikiwa ni pamoja na kuwa na hati sahihi, kuendeleza maeneo yale pamoja na kulipa kodi ya ardhi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Wizara ya Ardhi itaingilia kati usimamizi bora wa matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambayo inaendelea kushika kasi ndani ya Jimbo la Momba?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester.

Mheshimiwa Spika, napenda tu nimhakikishie; kwenye swali lake la kwanza anataka kujua nini tamko la Serikali kwa hawa wawekezaji ambao wanajichukulia sheria mkononi.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe rai tu kwa wananchi kuhusu namna ya uuzaji wa ardhi kwa wawekezaji. Tuwaombe sana, kwa sababu mara nyingi wawekezaji wanaenda moja kwa moja kwenye maeneo, wanaonana na watu bila kufuata taratibu na wanauziana bila kuzingatia sheria; na hatima yake anapokuwa amepewa hati yake wewe ulimuuzia hekari 100, anakuja na hati yenye hekari zaidi ya 100, ni kutokana na nyaraka ambazo zinatakiwa kuwepo kwa kuzingatia sheria yenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niwaombe, kwanza nitoe rai, kwamba, ili kuondoa hii migogoro uuzwaji wowote wa ardhi lazima uhusishe halmashauri husika ambao ndio wanaotambua mipaka yako na namna ambavyo mnaweza kuuziana ardhi kwa wawekezaji. Na wakati mwingine unaweza ukamuuzia mtu ambaye hata si raia wa Tanzania ilhali hairuhusiwi kwa raia wa kigeni kuweza kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la kodi ambazo hawalipi, tayari tulishaanza mkakati wa kuwafuatilia. Tunachohitaji tu ni halmashauri husika kuona ni namna gani pia ya kuanza ule mchakato wa kufuata sheria, taratibu zile za kutoa maonyo kuanzia kwenye Kifungu cha 45 mpaka 48 ambavyo vinaelekeza njia nzuri ya kuweza kumnyang’anya mtu hati yake hata kama amepewaa kisheria.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema ni lini Wizara itaingilia kati ili kumaliza migogoro hii ya wakulima na wafugaji. Tatizo hilo linaweza likaisha pale tu ambapo kijiji kitakuwa na mpango wa matumizi ya ardhi; na matumizi ya ardhi hayapangwi na Wizara, yanapangwa na maeneo husika. Kwa hiyo sisi kama Wizara intervention yetu inakuja pale ambapo tunakuja sasa kuridhia kile ambacho mnakubaliana katika kutenga maeneo. Kwamba wafugaji wanatengewa maeneo yao, wakulima maeneo yao, maeneo ya makazi nayo yanakuwepo. Kwa hiyo tunapokwenda sisi ni kuweka ile mipaka kwa ajili ya kuheshimu taratibu hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama vijiji hivi havijawa na mpango wa matumizi basi tunaielekeza pia Tume ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ikashirikiane na Wilaya ya Momba waweze kuweka matumizi ya ardhi katika maeneo yenye mgogoro. (Makofi)

Name

Dr. John Danielson Pallangyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Mashariki

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani kutatua migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi wa Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona, tatizo lililoko kule Momba linafanana sana na kule Arumeru Mashariki maeneo ya Kia kwenye mashamba ya Malula. Wakulima wa eneo lile walipewa notice na Serikali kwamba wataondolewa lakini wangefidiwa. Hata hivyo, kabla ya zoezi hilo kufanyika kukazuka mgogoro na wawekezaji hawajaonekana pia Serikali inasema kwamba wakulima wale wako pale kimakosa na mashamba yale yalikuwa ni ya Serikali. Je, ni lini Serikali itatoa tamko kuhusu wakulima wale kwamba watafidiwa au la au wataendelea na kufanya kazi zao za kilimo?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo kumekuwa na migogoro kati ya wawekezaji na wananchi maeneo mengi ambayo yana migogoro ni yale ambayo wawekezaji walipewa na wakayatelekeza mashamba yao matokeo yake wananchi wakawa wameingilia pale. Kisheria ni kwamba kama mtu amekaa pale kwa muda wa miaka 12 bila kusumbuliwa anakuwa na uhalali wa kuendelea kumiliki eneo lile kama katikati hapakuwa na mawasiliano ya kuweza kujua kwamba anadai eneo lake limevamiwa au namna gani. Sasa pale kama Serikali ilishaingia na kuwatambua kwamba wananchi wana haki basi hilo kwa sababu ndio nimelipata hapa, naomba nilichukue ili nifanye ufuatiliaji wa karibu kuweza kujua uhalisia wa kile anachokisema na hali halisi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia katika maswali haya hasa katika mashamba yaliyotelekezwa ni jukumu pia la mamlaka zenyewe za upangaji kufanya ufuatiliaji kuweza kufanya ukaguzi kuona mashamba yote yale ambayo yanamilikiwa na wawekezaji au hata kama ni mtu binafsi lakini amelitelekeza kwa maana ya kukiuka masharti yaliyoko kwenye hati yake, utaratibu wa kuanza kutaka kumnyanganya unaanzia kwenu kama halmashauri.

Kwa hiyo, wakishaleta sisi kazi ya Waziri ni kumshauri Mheshimiwa Rais kufuta pale ambapo anakuwa amekizi vigezo. Kwa hiyo, nitoe rai kwa halmashauri zote kule kuliko na mashamba pori ni jukumu la halmashauri sasa kuanza kufanya ufuatiliaji, ku-save notice, kutoa maonyo na mwisho wa siku wakipendekeza kufutwa Wizara itakuwa tayari kushirikiana nao kuhakikisha taratibu zinafuatwa, ahsante.