Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DOROTHY G. KILAVE Aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Buza/Nzasa – Kilungule pamoja na daraja litamalizika hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo inawaunganisha wananchi wa Temeke na Mbagala?

Supplementary Question 1

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, miaka ya mwanzo ya 2000, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi ilikuwa na miradi ya viwanja 20,000, ambapo kwenye Jimbo la Kawe ilihusisha Kata ya Mbweni na Kata ya Bunju.

Mheshimiwa Spika, wananchi wakati wanalipia viwanja moja kati ya ahadi ya Serikali ilikuwa ni kutengeneza barabara za ndani. Hata hivyo, mpaka sasa hivi barabara nyingi za ndani za Kata hizi za Mbweni na Bunju kwenye mradi wa viwanja 20,000 bado ipo katika hali mbaya. Ninataka tu commitment ya Serikali kama itaenda kufanya uchunguzi na kuweza kwenda kufanya utaratibu wa kutengeneza barabara moja baada ya nyingine, kwa sababu wananchi walilipia kwenye viwanda.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima James Mdee kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alichokuwa anakitaka hapa ni ahadi ambayo ilitolewa na Serikali katika miaka ya 2000 ya kutengeneza barabara za ndani katika maeneo ya Bunju na Vijibweni. Mimi nimwambie tu kwamba tumepokea kile alichokisema, kwamba anataka commitment ya Serikali, na sisi tunakubali kwenda maeneo hayo, tutakwenda kufanya tathmini kujionea hali ili tuone na bajeti jinsi ambavyo tutakavyopanga kutekeleza ahadi ya Serikali ambayo ilikuwa imepangwa kwa wakati huo. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nimfahamishe Mheshimiwa Mdee kwa swali lake kwamba, ni kweli mradi huo ulikuwepo, lakini baadaye miradi yote kutoka kwenye Wizara tumeirudisha kwenye mamlaka za upangaji. Kwa hiyo ni jukumu pia la Halmashauri husika kuwasiliana na watu wa TARURA kwasababu zile zinakuwa zipo chini ya TARURA ili TARURA waweke kwenye mpango ili ziweze kufunguliwa kama ambavyo ilistahili kuwa.