Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA Aliuliza:- Akina mama wajawazito wamekuwa wakitozwa fedha kuanzia shilingi 50,000/= hadi 70,000/= wasipojifungulia katika Vituo vya Afya hasa katika Jimbo la Kalenga; huku vituo hivyo vikiwa mbali na maeneo wanayoishi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga maeneo ya kusubiri kujifungua katika Vituo vya Afya?

Supplementary Question 1

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa sehemu za kujisubiria akina mama hasa wajawazito. Tumesema katika sera kwamba tutakuwa na Vituo vya Afya katika kila Kata na Zahanati katika kila kijiji; lakini katika Jimbo la Kalenga hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Akina mama wakijifungulia njiani wanatozwa Sh.50,000/= mpaka Sh.70,000/=. Ni lini Serikali itajenga majengo ya kujisubiria katika Jimbo hili la Kalenga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini kauli ya Serikali kuhusu hizo tozo ambazo zinatozwa kwa akina mama ambao pia ni walipa kodi katika nchi hii na Serikali ndiyo yenye changamoto ya kutojenga hivyo Vituo vya Afya? (Maikofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Tendega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunahitaji kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga kwa kuboresha miundombinu ya huduma za afya. Ni kweli kwamba miradi ya ujenzi wa majengo ya kujisubiria kwa maana ya maternity waiting homes, imekuwa ni kipaumbele cha Serikali. Hata hivyo, majengo hayo yanajengwa ili kupunguza umbali wa wajawazito kufika kwenye Vituo vya Huduma za Afya. Kwa hiyo, ili ujenge majengo haya ni lazima uwe na Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Spika, sasa kupanga ni kuchagua. Ndiyo maana Serikali imepanga kwanza kujenga kwa wingi Vituo vya Afya ili viwe karibu zaidi na makazi ya wananchi na tuweze sasa, yale maeneo ambayo yana umbali mkubwa, kuweka mpango wa pili wa kuanza kujenga majengo ya kujisubiria wajawazito. Haitakuwa na tija sana ukiwekeza kujenga majengo ya kujisubiria wananchi sehemu ambayo ina umbali mkubwa sana kutoka kwenye vituo vya huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kipaumbele namba moja ni lazima uwe na kituo, ndiyo maana yale majengo yanajengwa karibu na kituo. Ndiyo maana katika miaka hii mitano tumejenga vituo vingi na tunaendelea na ujenzi wa vituo hivyo ili kusogeza huduma kwa wananchi, hatimaye tutakuja kujenga sasa majengo ya kusubiria wajawazito. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipaumbele hicho bado kipo, lakini tunaboresha kwanza vituo na baadaye tutakenda kwenye awamu wa ujenzi wa majengo ya kujisubiria.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kauli ya Serikali kuhusu tozo, Serikali haijatoa maelekezo yoyote kwa watendaji na watoa huduma kutoza faini kwa wajawazito wanaojifungulia majumbani.

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ni wajibu wa watumishi katika vituo vya huduma kutoa elimu na kuhamasisha wajawazito kuona umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya huduma badala ya kuwalipisha faini wakijifungulia nje ya vituo vya huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea kusimamia jambo hilo. Naomba nitoe wito kwa watendaji wote kuzingatia jukumu lao la kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujifungua katika vituo vya huduma.

Name

Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA Aliuliza:- Akina mama wajawazito wamekuwa wakitozwa fedha kuanzia shilingi 50,000/= hadi 70,000/= wasipojifungulia katika Vituo vya Afya hasa katika Jimbo la Kalenga; huku vituo hivyo vikiwa mbali na maeneo wanayoishi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga maeneo ya kusubiri kujifungua katika Vituo vya Afya?

Supplementary Question 2

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hospitali nyingi zinatoza wanawake wajawazito wanapokwenda kujifungua. Hospitali ya Kitete ni moja kati ya Hospitali ambazo zinatoka akina mama; anapojifungua mtoto wa kiumbe analipa Sh.50,000 na anapojifungua mtoto wa kike, analipa Sh.40,000. Je, Serikali imeweka tozo hii kwa ajili ya nini? (Kicheko/Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma za afya nchini unatolewa kwa mujibu wa sheria, sera na miongozo ikiwemo utoaji wa huduma za afya kwa wajawazito wakati wa kujifungua. Serikali imeelekeza bayana kwamba huduma za wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano zinatolewa bila malipo yoyote na Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na miongozo hiyo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya maeneo, kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu, kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wanatekeleza kinyume na sera na mwongozo huo. Kazi ya Serikali ni pamoja na kupokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niyachukue mawazo ya Mheshimiwa Mbunge na niwahikikishie kwamba tutaenda kuyafanyia kazi ili kuondokana na changamoto hiyo. (Makofi)